November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCB,yabuni mbinu mpya kuongeza uzalishaji zao la pamba

Na. Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Katika kuhakikisha wakulima wanaongeza kasi ya uzalishaji wa zao la pamba na kuondokana na umasikini,Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imeandaa mkakati wa elimu endelevu itakayowasaidia kufanya kilimo cha kisasa cha tija na chenye kuzingatia kanuni 10 za kilimo.

Mkaguzi wa Pamba, Daniel Bariyanka, wa TCB akiwaeleza vijana waliotembelea banda la bodi hiyo katika maonesho ya Nane Nane yanayofanyika Nyamh’ongolo wilayani Ilemela jijini Mwanza, yakiwashirikisha wakulima, wavuvi na wafugaji wa Kanda ya Ziwa Magharibi.

Akizungumza katika maonesho ya kilimo ya Nane Nane Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika uwanja wa Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza ,Mkaguzi wa Pamba wa TCB,Daniel Bariyanka,amesema kanuni ziko katika Sheria Namba 2 ya Pamba ya mwaka 2001 ambazo zilitungwa mwaka 2011.

Hivyo wanachofanya ni kuzitafsiri,zinafikaje na kwa kiwango gani kwa wakulima,ingawa walio wengi wamepata elimu ya kilimo bora kupitia mikutano kati ya Maofisa Ugani,wataalamu wa TCB,vyombo vya habari,wakulima wenyewe na wadau wa mnyororo wa thamani wa pamba.

Amesema kuwa utekelezaji wa kanuni hizo baadhi zinaeleweka kwa asilimia 100,zingine bado hasa zinazomtaka mkulima azalishe kwa tija,hawana umakini wa kuzifuata wakidai ni kazi ngumu ila upandaji na vipulizi sahihi wanaendelea kufanya,waliozingatia wamefanikiwa na matokeo ni mazuri.

Mkaguzi wa Pamba, Daniel Bariyanka TCB akiwaeleza vijana waliotembelea banda la bodi hiyo katika maonesho ya Nane Nane yanayofanyika Nyamh’ongolo wilayani Ilemela jijini Mwanza, yakiwashirikisha wakulima, wavuvi na wafugaji wa Kanda ya Ziwa Magharibi.

Hata hivyo amesema bodi hiyo imejipanga kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuanzisha mashamba darasa yatakayofikisha elimu kwa upana kupitia kila vitongoji na vijiji katika maeneo yatakayoonyesha umuhimu wa upandaji kwa vipimo vipya vya sm 60.

Mkakati unaandaliwa wa vi-plot (vishamba)vitatu vya kupanda kwa kumwaga mbegu,vipimo vya zamani vya sm 90 kwa sm 40 na vipimo vipya vya sm 60 kwa sm 30 kati ya mstari na mstari ambapo amesema wanaamini mashamba darasa hayo ngazi ya vijiji na vitongoji,wakulima watashiriki moja kwa moja kwa sababu watakuwa wanakwenda shambani kujifunza moja kwa moja.

“Mkakati huu wa mashamba darasa utaanza kipindi cha kiangazi,yatamwagiliwa sawa na yaliyopo katika maonesho na mkulima atakuwa na uwezo wa kuyahudumia kwa kumwagilia maji hadi Novemba 15 msimu unapoanza watakuwa wameshajifunza kanuni 10 bora za kilimo kupitia mashamba hayo,”.

Aidha alifafanua sababu za uzalishaji wa pamba umekuwa ukipanda na kushuka hiyo yote ni kutokana na mabadiliko ya tabianchi,mvua zinaponyesha kubwa zinaathiri uzalishaji huku ukame pia ukichochea kuharibu kutokana na zao lenyewe kutokuwa na mfumo wa umwagiliaji.