December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo:Serikali ichukue mawazo yenye tija kuingiza katika uboreshaji wa mkataba

Judith Ferdinand na Daud Magesa, Mwanza

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza serikali kuruhusu mawazo yenye tija katika uwekezaji wa bandari kuingizwa katika uboreshaji wa mkataba huo ili kuwafikisha katika kiwango wanacho taka.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo,wakati akizungumza na wanaCCM na wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa,wakati hakihitimisha mkutano wa hadhara wa kuelimisha wananchi juu ya mkataba wa uwekezaji wa bandari,uliofanyika uwanja wa CCM Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo, akizungumza na wanaCCM na wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa CCM Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza

“CCM inasisitiza uwekezaji ndio,hatua zinazoendelea ndio lakini kama kuna mtu ana maoni yenye tija yaongezwe ili tupate na tufike kwa kasi kule tunapopataka kwani mkataba siyo msaafu useme kuwa hauna dosari kwani imeandikwa na binadamu,”amesema Chongolo.

Chongolo amesema msimamo wa CCM katika uwekezaji wa bandari ya Dar-es-Salaam ni kasi ya utekelezaji uongezewe ili waweze kupata manufaa kwa haraka.

“Msingi wa utekelezaji wa uwekezaji huo ni Ilani ya CCM ambayo tuliinadi mtu akitaka kuwakwamisha utekelezaji wa Ilani yetu hatupo tayari tunakuwa kitu kimoja,kwani ilani yetu ibara ya 22 na 59 inaeleza suala la uwekezaji huo kwa kina,”amesema Chongolo.

Sanjari na hayo amewaonya wapotoshaji na kuwataka kuacha kuitukana serikali na kuichonganisha na wananchi kwa mambo yasiyo ya msingi kwani CCM haina muda wa kuhangaika na matusi hayo, ikifanya hivyo itaondoka kwenye reli na kushindwa kuwahudumia wananchi.

“Wanao watukana msiwajibu kwa matusi kwani watawaondo kwenye reli sisi tunawajibu kwa utekelezaji wa Ilani kwa kufanya maendeleo ya miradi kwa wananchi,”.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Steven Wasira,ameshukia mitandao ya kijamii akiituhumu kukuza jambo la uwekezaji wa bandari na kuwataka wananchi waipuuze huku akiifananisha na bomba linalosafirisha majitaka na kuwataka wananchi wachukue mazuri ya mitandaoni na kuyaacha mabaya.

Wasira amesema katika maeneo yote waliyopita nchini hakuna mahali wananchi hawataki uwekezaji huo na hao wanaopinga ni sawa na maharage yasiyoiva unaweza kuyatoa ukaendelea kupika,kuwekeza ni jambo la lazima kwa mtu anayetaka faida na kukuza mtaji.

Amesema kwa kuwa bandari ni chombo biashara licha ya kuwa ni mpaka lazima ufanyike uwekezaji wa tija na siyo kwamba bandari inauzwa na hakuna bandari itakayouzwa hata hapa Mwanza, na wanaosema imeuzwa je,imeuzwa kwa shilingi ngapi?.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo ameupongeza uongozi wa CCM kutafsiri vizuri uwekezaji wa bandari na kuwafikia wananchi wengi.

Amesema uwekezaji wa bandari una mambo mawili,mpaka na biashara ya kupakia,kuhifadhi na kupakua mizigo,kwa sera ya nchi kazi hiyo hufanywa na sekta binafsi huku usalama ukibaki serikalini, uendeshaji na usimamizi ukifanywa na TPA.

Amesema umiliki wa bandari ni jukumu la serikali hauihusu sekta binafsi hivyo bandari zote zitaendelea kumilikiwa na serikali kwa mujibu wa Sheria Namba 4 ya Ardhi.

“Mbunge mwenye akili kabla ya kupitisha jambo lazima atafakari na kujiridhisha.Kwa nini wabunge waliunga mkono uwekezaji wa bandari, walifanya hivyo kwa sababu ni wawakilishi wa wananchi,walihakikisha mkataba una maslahi na manufaa ya nchi,wananchi na majimbo yao,”amesema Profesa Mkumbo.

Amesema serikali haina kiwanda cha kutengeneza fedha bali kodi kutokana na uwekezaji,hivyo wabunge waliunga mkono mkataba baada ya kuona una tija na faida nyingi za kuongeza ajira kwa vijana kutoka 29,000 hadi 70,000 waingie katika shughuli za uchumi katika sekta ya usafirishaji,wapate kipato wasiwe mzigo wawasaidie wazazi.

“Tumewaacha wanasheria wabishane ila tunawaambia waweke sheria vizuri uwekezaji wa bandari ufanyike,ili kuwaondoa wananchi hofu na mashaka kwamba mwekezaji DP World hakuwa na washindani,serikali ilala akaibuka Waziri Profesa Makame Mbarawa,si kweli.”

“Kulijitokeza kampuni saba za wababe waliobobea ambazo zilipambanishwa kwa kuangalia uwezo na uzoefu wa kufanya shughuli za bandari Ambapo DP World iliibuka mshindi,”ameeleza Profesa Mkumbo.

Alisistiza kuwa licha ya serikali kufanya uwekezaji mkubwa,bado bandari zetu ufanisi wake ni mdogo,ili kuchangamsha shughuli za kiuchumi bandari ya Dar es Saalam ikizubaa na zingine zitazubaa hivyo lazima iboreshwe iwe na manufaa.

Profesa Mkumbo alieleza kuwa bandari zote za TPA mwaka wa fedha ulioisha ziliingiza sh. bilioni 795.2 na matumizi yakiwa ni zaidi ya bilioni 791 ambapo TRA ilikusanya trilioni 7.76 hivyo mwekezaji anatarajia kuongeza mapato ya trilioni 26 na tutaongeza mapato ya ndani na kuiwezesha serikali kutoa huduma za jamii.

“Bajeti yetu ni trilioni 44.36 fedha hizo zinatoka wapi,TRA inakusanya trilioni 26 bado makusanyo hayazikidhi,zinabaki trilioni 18, ni lazima tutafute mkopo na wabunge watafute vyanzo vipya vya mapato,”ameeleza na kuongeza kuwa

“Tukiwekeza bandari ya Dar es Salaam na kuweka mazingira mazuri ya kupokea mizigo tukawashawishi majirani zetu tutaongeza uwezo wa serikali kuhudumia jamii,”amesema.

Profesa Mkumbo amesema wana uzoefu wa uwekezaji zaidi ya miaka 30 kila uwekeaji mpya unapoletwa kumekuwa na maswali na wasiwasi na yawezekana wasiwasi ni akili,hivyo serikali na Bunge watazingatia maoni na kuondoa hofu na wasiwasi uliopo kwani tuna uzoefu wa kuhakikisha maslahi ya wananchi yanazingatiwa.