Na Esther Macha, Timesmajira Online,Mbeya
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ameagiza kufungwa mara moja nyumba ya wageni inayomilikiwa na askari PC John Kaijage ijulikanayo kama Govenor iliyopo Iwambi ambako mwendesha bodaboda aliuwawa.
Chalamila amesema hayo jana wakati wa kuaga mwili wa Marehemu Erasto Mwalwega (29) aliyeuwawa na askari polisi na wenzake watatu katika nyumba ya kulala wageni itwaayo Govenor iliyopo Iwambi.
Chalamila amesema kwamba vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari wasio waadilifu ambao hujichukulia sheria mkononi kwa kuwanyanyasa raia si vizuri, na kwamba dhamana waliyopewa ni kuwatumikia wananchi na si kuwanyanyasa kwa vipigo na rushwa.
“Hivi karibuni nimeamuru raia kurejeshewa fedha zao milioni moja la laki tano zilizoporwa na mmoja wa askari Polisi” amesema Chalamila na kuwapongeza madaktari waliouchunguzi mwili wa marehemu ambapo amesema alifariki kutokana na kipigo.
Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson ambaye ni mlezi wa bodaboda jijini Mbeya amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na askari kwani wananchi tegemeo lao ni askari, sasa vitendo viovu vinapofanywa na askari vinawapa wakati mgumu kama raia.
Dkt. Tulia amemuomba Kamanda wa Polisi kusimamia na kuhakikisha kesi inaendeshwa vizuri bila upendeleo na hatapenda kusikia mtuhumiwa yupo mitaani eti kwa sababu aliyefanya kosa ni askari.
Dkt Tulia amehitimisha kwa kutoa ubani kwa mjane wa marehem ambaye amemwacha akiwa na mtoto mmoja.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amewatoa hofu wananchi na kwamba jeshi hilo halikusita kuchukua hatua haraka kwa kumkamata ntuhumiwa na kumuweka mahabusu.
“Taarifa za kuwa mtuhumiwa analala nyumbani si za kweli na kwa kauli hiyo naenda kuongeza kufuli jingine mahabusu” amesema Matei.
Marehemu alifariki baada ya kupigwa maeneo mbalimbali ya mwili wake na kusababisha damu kuvilia katika ubongo. Mwili wa marehemu ulisafirishwa kwenda Masoko kwa ajili ya mazishi.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi