November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Mwanza yawapandisha kizimbani watumishi wawili wa Tanesco kwa tuhuma za uhujumu uchumi

Na.Daud Magesa, Timesmajira Online, Ilemela

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza,imewafikisha mahakamani watumishi wawili wa Shirika la Ugavi la Umeme Tanzania (TANESCO) wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 5 ya 2023 na kuisababishia serikali hasara zaidi ya bilioni 2.

Watumishi hao ni Fundi Mchundo ambaye ni Abdulkadri Hussein (39) na Ofisa Bohari wa shirika hilo,Respicius Rumanyika (33), walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza,jana na kusomewa mashitaka 125 yaliyogawanywa katika makundi matano.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Stella Kiama,Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali,Magreth Mwaseba akisaidiana Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, Maximillian Kyabona,amesema washitakiwa hao wanashitakiwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2022 Sura ya 200.

Mwendesha mashitaka huyo aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa wa kwanza,Abdulkadri Hussein na mshitakiwa wa pili,Respicius Rumanyika,kwa nyakati tofauti walitenda makosa hayo kati ya Novemba 16,2022 na Disemba 17, 2022, huko Nyakato katika Bohari la Tanesco,Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza.

Mwaseba alidai washitakiwa wakiwa watumishi wa umma waliongoza genge la uhalifu,wizi wa vifaa vya miundombinu ya umeme,kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo,ubadhirifu na kuisababishia serikali hasara zaidi ya sh.bilioni 2.

Mwendesha Mashitaka huyo Mwandamizi wa Serikali alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo unaendelea na washitakiwa hawatakiwi kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi,hivyo aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili Eric Mutta anayemtetea mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo (Abdulkadri),amesema kwa vile upelelezi haujakamilika wanakusudia kuwasilisha maombi ya dhamana kwa wateja wao ambapo mshitakiwa wa pili anatetewa na Wakili Linus Amri.

Akiahirisha shauri hilo Hakimu wa Mahakama hiyo, Kiama amesema kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo la Uhujumu Uchumi,washitakiwa wataendelea kubaki mahabusu hadi Agosti 10,mwaka huu,kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Aidha Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, Kyabona, akizungumza nje ya mahakama amesema watumishi hao wa TANESCO walifikishwa mahakamani hapo na kuwasomea mashitaka ya uhujumu uchumi yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kuhujumu vifaa vya miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Mwanza.