Na Suleiman Abeid na Judith Ferdinand,
Timesmajira Online, Mwanza
SARATANI ya mlango wa kizazi imetajwa kuwa ni moja ya magonjwa hatari yanayochangia kupoteza maisha ya wanawake wengi hapa nchini.
Ugonjwa huo umetajwa kutokuwa na tiba pindi unapokuwa umempata mtu na kwamba kinga yake ni watoto wa kike kuchanjwa chanjo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo pindi wanapokuwa na umri wa miaka 14.
Hali hiyo imebainishwa na Ofisa Mipango wa Taifa wa chanjo kutoka Wizara ya Afya, Lotalis Gadau kwenye semina ya siku moja kuhusu masuala ya chanjo kwa waandishi wa habari kutoka mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Shinyanga, Mwanza na Simiyu iliyofanyika jijini Mwanza.
Gadau amesema ili kukabiliana na hali ya kupatwa na ugonjwa huo ni watu kuchanja chanjo ya kuzuia saratani hiyo (HPV) kwa mabinti wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 14 kwa waliovuka umri huo kuwa na utaratibu wa kuchunguzwa afya zao kila baada ya kipindi fulani.
“Saratani ya mlango wa kizazi ni ugonjwa hatari ambao mpaka sasa hauna tiba ni vyema tuhamasishe mabinti zetu wenye umri kati ya miaka tisa hadi 14 kuchanjwa chanjo hii ya HPV ili kuondoa uwezekano wa kupatwa na janga hili,” amesema na kuongeza kuwa
“Lakini vilevile kwa wanawake ambao tayari wamevuka umri wa miaka 14 ni vyema wakawa na utaratibu wa kuchunguzwa na wataalamu ili kubaini hali zao, na hata kama ikibainika kuwa na dalili za ugonjwa huo inakuwa rahisi kupatiwa tiba na mtu kupona kabisa,”amesisitiza.
Amesema changamoto inayojitokeza ni watu kutokuwa na utamaduni wa kuangalia afya zao, inapotokea maambukizi kuwa ya muda mrefu tayari wanakuwa wameisha athirika hivyo matokeo yake yanakuwa si mazuri.
Pia amesema mpaka hivi sasa inahisiwa mabinti 541,232 hawajapata chanjo hiyo ya kinga ya saratani ya mlango wa kizazi ambapo Mkoa wa Tabora ukitajwa kuongoza hapa nchini kutokana na kuwa na mabinti wapatao 55,157 ambao hawajapatiwa chanjo hiyo ya HPV.
“Mpaka hivi sasa Wizara yetu ya Afya imekuwa ikitoa chanjo mbalimbali hasa kwa watoto, mabinti na akina mama wajawazito,miongoni mwa chanjo hizi ni pamoja na chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV), Uviko-19, kifua kikuu (BCG), polio (IPV), surua na rubella (MR), Dondakoo, kifaduro, pepopunda, homa ya ini, uti wa mgongo, homa ya mapafu (Pentavalent),pneumonia (PCV13) na kuharisha kukali (rota),” ameeleza Gadau.
Sanjari na hayo amesema waandishi wanapaswa kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kupatiwa chanjo za kinga kwa magonjwa mbalimbali ili kuepuka kupatwa na magonjwa hatari ambayo miongoni mwake hayana tiba mpaka hivi sasa huku ugonjwa Uviko-19 ulichangia chanjo nyingine kusahaulika.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja kwa waandishi wa habari mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Claudia Kaluli amewataka waandishi wa habari nchini waendelee kuandika habari zinazoihamasisha jamii kuona umuhimu wa kuzingatia suala la chanjo.
Kaluli amesema mpaka hivi sasa waandishi wa habari wamekuwa na mchango mkubwa katika kuielimisha jamii juu ya madhara ya magonjwa mbalimbali na umuhimu wa kupatiwa chanjo ya kinga ya magonjwa ambayo baadhi yake hayana tiba mpaka hivi sasa.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru waandishi wa habari kwa juhudi zenu mnazozifanya katika kuwahabarisha watanzania masuala mbalimbali muhimu ikiwemo upande huu wa sekta ya afya na chanjo, mmekuwa na mchango mkubwa sana maana wananchi wengi wanaviamini vyombo vya habari,” ameeleza Kaluli.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) saratani ya mlango wa kizazi huwaathiri zaidi ya wanawake nusu milioni kila mwaka na kusababisha vifo vya wanawake 250,000 hali inayohitajika watu kuelimishwa zaidi ili mabinti wenye umri wa miaka 14 wachukue hatua za kupata chanjo ya HPV.
Katika maelezo yake kwa mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Afya, Catherine Sungura amesema Wizara ya Afya imekuwa ikitoa mafunzo kwa waandishi wa habari hapa nchini ili kuwajengea uwezo zaidi katika kuandika habari zinazohusu masuala ya afya ikiwemo chanjo mbalimbali.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa