November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi binafsi Korogwe walia na shida ya maji

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

BAADHI ya taasisi binafsi ikiwemo shule ya mchepuo wa kingereza ya Good Foundation iliyopo Kata ya Bagamoyo katika Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga wamelalamikia shida ya maji kwenye mji huo.

Wadau hao wamelalamika kuwa, pamoja na Mto Pangani kupita katikati ya Mji wa Korogwe bado shida ya maji ni kubwa, wamelazimika kuchimba kisima cha maji ili kuweza kukidhi mahitaji ya maji kwa wanafunzi wanaoishi bweni na wale wa kutwa.

Wahitimu wa darasa la saba shule ya mchepuo wa kingereza ya Good Foundation iliyopo Kata ya Bagamoyo, Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga wakiingia ukumbini kwenye mahafali ya 10 ya shule hiyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Good Foundation Profesa Elifas Bisanda kwenye mahafali ya 10 ya darasa la saba ya shule hiyo yaliyofanyika Julai 16, 2023, ambapo wanafunzi 33 walihitimu elimu hiyo kati yao wavulana ni 15 na wasichana 18.

“Moja ya changamoto ni kukosekana maji safi ya bomba Mamlaka ya maji katika Halmashauri ya Mji Korogwe, imeshindwa kusambaza maji katika mji wetu, hasa huku Bagamoyo licha ya kuwepo chanzo kikubwa cha maji yaani mto Pangani na mfumo wa maji tayari umeshaunganishwa shuleni, ingawa maji hayajatoka, tunategemea maji ya kisima kirefu kilichochimbwa na shule,”.

Pia ameishukuru TANESCO na REA kwa kuwaunganishia umeme unaowasaidia kusukuma maji hayo kwa urahisi zaidi.

Mkurugenzi wa Shule ya Good Foundation ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Profesa Elifas Bisanda akipanda mti kwenye shule hiyo katika mafahali ya 10 y shule hiyo.

Profesa Bisanda ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),amesema changamoto nyingine ni kupata walimu wenye weledi na viwango vinavyoendana na mfumo wa English Medium.

“Hivi sasa bado tunawategemea sana walimu wastaafu ambao hata hivyo wengi wamechoka sana,tunajitahidi kukabili uhaba wa walimu wa hisabati na sayansi, na hivi sasa masomo hayo tuko vizuri sana. Bila shaka mwaka huu tutafanya vizuri zaidi katika mitihani ya Taifa,”amesema Profesa Bisanda.

Amesema changamoto nyingine ni wazazi wanaopeleka watoto shuleni hapo lakini wakashindwa kulipa ada kwa wakati kwani shule haina chanzo kingine cha mapato mbali na ada, inawawia vigumu kulisha wanafunzi, kulipa mishahara ya walimu na wafanyakazi wengine pamoja na kulipa kodi mbalimbali.

Mgeni rasmi kwenye mahafali ya 10 ya Shule ya Good Foundation Mhandisi Mugisha Bisanda ambaye ni Afisa Mkuu wa Ufundi wa Kampuni ya Ericson hapa Tanzania, akizungumza kwenye mahafali hayo.

Profesa Bisanda amesema mafanikio ya shule hiyo si katika ufaulu wa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi peke yake bali ni pamoja na msingi mzuri waliowawekea wahitimu hao wakiwemo wale ambao tayari walishamaliza hapo na kujiunga na sekondari kwenye shule za vipaji kama Ilboru, Tanga Technical, Ifunda, Mtwara Technical, Kilakala na Mzumbe.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Zebadia Maanga amesema mwaka 2022, shule hiyo imepeleka wanafunzi wawili msichana na mvulana shule za vipaji ambazo ni shule ya sekondari ya Wasichana Kilakala na shule ya sekondari ya Wavulana Mzumbe zilizopo mkoani Morogoro.

“Hata hivyo, katika wanafunzi kumi bora katika Halmashauri ya Mji Korogwe yenye jumla ya shule 33, wanafunzi watano bora waliohitimu mtihani wa utimilifu wa kumaliza elimu ya msingi 2022 walitoka Good Foundation School.

Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, Mhandisi Mugisha Bisanda ambaye ni Ofisa Mkuu wa Ufundi wa kampuni ya Ericson hapa Tanzania aliwata wanafunzi hao kuitumia elimu waliyoipata kuwa chachu ya kuwawezesha kufanya vizuri kwenye elimu ya sekondari na vyuo vikuu.

Huku akiwasihi wasijiingize kwenye vitendo viovu kama michezo ya kamari, ulevi, uvutaji wa tumbaku, bangi na matumizi ya dawa za kulevya.

Amesema vijana wengi wamejikuta wakinaswa na matumjzi ya bangi na dawa kama cocaine, heroin na mandrax na kusababisha kupata magonjwa ya akili na wengine kuishi kama vibaka mtaani na mwisho wanakufa mapema.