Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula, ameeleza kuwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Disemba 2022 katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kwa Jimbo hilo halmashauri ya Ilemela katika sekta ya elimu imefanikiwa kujenga shule mpya 5 za sekondari,2 za msingi pamoja na madarasa 207.
Dkt.Angeline amebainisha hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Ilemela kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Disemba 2022 katika mkutano mkuu wa CCM Wilaya ya Ilemela uliofanyika Julai 18,2023 katika uwanja wa CCM Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Ambapo ameeleza kuwa katika kipindi hicho cha miaka miwili hadi kufikia Machi 2023 Jimbo na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imepokea zaidi ya bilioni 46 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ameeleza kuwa sekta ya elimu katika halmashauri hiyo na Jimbo hilo imefanikiwa kuanzisha na kufungua shule 5 mpya za sekondari ambazo ni Buzuruga,Igongwe,Semba, Nyamh’ongolo na Lubuka pamoja na kufunguliwa kwa shule 2 mpya za msingi za Bujingwa na Buyombe.
“Katika kipindi hicho Halmashauri kwa kupitia mpango wa maendeleo (UVIKO-19) na pochi ya mama imewezesha kujenga na kukamilisha madarasa 207 kwa ajili ya kidato cha kwanza mwaka 2023 huku ilifanikiwa kujenga nyumba 2 za walimu (2in1) katika shule za msingi Isanzi na Hekima pamoja na ukamilishaji wa bweni shule ya sekondari ya wasichana Bwiru,”ameeleza Dkt.Angeline.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa katika kipindi cha Novemba 2020 Hadi Desemba 2022 ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo imeendelea kutoa msaada wa kimasomo kwa watoto yatima na walioa katika mazingira magumu kwa kadri inavyojaliwa katika suala la fedha.
“Jumla ya watoto watano niliwapeleka chuo cha Tandabui kwa ajili ya masomo ya unesi,famasia,clinical Officers na maendeleo ya jamii ambao wanaendelea vizuri isipokuwa mmoja kutoka Kata ya Bugogwa ambaye kwa bahati mbaya alifukuzwa kwa kesi ya kukosa uaminifu katika chumba mtihani,”ameeleza Dkt.Angeline na kuongeza kuwa
Pia katika sekta ya afya Halmashauri imeweza kukamilisha na kufungua zahanati 3 ambazo ni Lumala,Masemele na Nyamadoke ili kutanua wigo wa utoaji huduma za afya huku katika kuboresha huduma ya mama na mtoto imekamilisha majengo ya kujifungulia katika zahanati ya Nyakato na Ilemela.
Vilevile kupitia mapato ya ndani halmashauri hiyo imeendelea na ukamilishaji wa jengo la kujifungulia katika zahanati ya Nyamwiholela na Ilemela.
“Halmashauri imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa kituoa cha afya Kayenze na majengo muhimu ya hospitali ya Wilaya na huduma za wagonjwa wa nje zinazotolewa huku imetumika fedha zake za ndani kujenga wodi ya kina mama katika kituo cha afya cha Buzuruga na zahanati ya Nyakato,”ameeleza Dkt.Angeline.
Aidha ameeleza kuwa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na ofisi ya Mbunge wanefyatua tofali 76,335 na kuzigawa katika taasisi za serikali kama vile shuleni, zahanati ikiwemo ya Lumala, Masemele na Nyamadoke.
Mbali na hayo ameeleza kuwa katika suala la utunzaji wa mazingira halmashauri hiyo imefanikiwa kupanda miti 50,500 katika taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo hospitali ya Wilaya,vituo vya afya,zahanati pamoja na shule za msingi na sekondari.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â