November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Juhudi bado zinahitajika mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Na Suleiman Abeid, Timesmajira Online


NOVEMBA 25 hadi Desemba 10 ya kila mwaka mataifa yote ulimwenguni huadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Maadhimisho ya siku 16 yalianzishwa rasmi mnamo mwaka 1991 ambapo mwaka huu wa 2023 yatatimiza miaka 32 yakiwa na lengo kuu la kupinga ukatili na kuweka mikakati mbalimbali ya jinsi ya kutetea haki za wanawake na watoto.


Kwa kawaida wiki hii utawaliwa na matukio na makongamano mbalimbali yenye lengo la kupaza sauti katika kupinga vitendo vya ukatili wa kinjisia huku mafunzo yakitolewa katika maeneo mbalimbali nchini ya kuielimisha jamii juu ya madhara ya vitendo hivyo.


Tunapozungumzia vitendo vya ukatili, tunamaanisha ni kitendo chochote anachotendewa mtu kitakacho msababishia madhara ya kimwili, kiakili au kisaikolojia.

Ni vitendo vyenye kusudio la kulazimisha au kutisha mtu hivyo kujikuta akifanya jambo kinyume na matakwa yake.


Mara nyingi waathirika wa vitendo vya ukatili nchini Tanzania huwa ni wanawake na watoto ambao takwimu zinaonesha ndiyo wanaoongoza kutendewa vitendo hivyo japokuwa katika miaka ya hivi karibuni imebainika pia kuwepo kwa wanaume wanaotendewa ukatili na wenza wao.


Kiuhalisia ukatili umegawanyika katika makundi makuu takribani manne ikiwemo ukatili wa kimwili, kingono, kiuchumi na kisaikolojia au tunaweza kusema wa kihisia.


Pamoja na kampeni mbalimbali zinazoendelea kufanyika nchini hapa kwa lengo la kupiga vita vitendo vya ukatili, lakini bado kasi ya upunguaji wa vitendo hivyo ni ndogo kutokana na baadhi ya watu kuuona ukatili mwingine kama jambo la kawaida kufanyika miongoni mwa jamii.


Baadhi ya vitendo vinavyoonekana kuwa ni vya kawaida ni ukatili wa kisaikolojia ambao mtu hufanyiwa huku jamii ikiona mfano, kutukanwa, kufanyiwa dhihaka, kudhalilishwa, vitisho vya kuuawa, wivu wa kupindukia, kunyimwa mafunzo,gubu na kupitia ujumbe mfupi (sms) kwenye simu unaomdhalilisha au kutisha mtu.


Jamii kuendekeza mila na desturi kandamizi ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuendelea kufanyika kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia miongoni mwa makabila hapa nchini mfano, mwanamke aliyefiwa na mumewe kulazimiswa kuolewa na ndugu wa mme pasipo ridhaa yake.


Tabia ya mwanamke kulazimishwa kurithiwa na ndugu wa mwanamume aliyefariki ni miongoni mwa mila za kiafrika ambazo baadhi ya makabila nchini hapa wanaziendeleza hali hii huwaathiri kisaikolojia wanawake wengi na wakati mwingine kuambukizwa magonjwa bila ya wao kutarajia.


Vile Tanzania bado inakabiliwa na wimbi kubwa la ukatili dhidi ya watoto chini ya umri wa miaka 18 hasa watoto wa kike ambao miongoni mwao hufanyiwa ukatili wa kunyimwa elimu kwa lengo tu la wazazi wao kutaka waolewe ili wapate mali zinazotolewa kama mahari.


Mbali na ndoa za utotoni lakini pia bado lipo wimbi kubwa la watoto kubakwa au kulawitiwa na kusababishiwa madhara makubwa ikiwemo kupata maambukizi ya virusi vinavyosababisha ukosefu wa kinga mwilini (UKIMWI) na mimba katika umri mdogo.


Tukumbuke kuwa haki za watoto zinalindwa katika mikataba mikubwa miwili ya haki za watoto, ambayo ni Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa mwaka 1990, yote ikiwa imeridhiwa na nchi yetu ya Tanzania.


Kwa Tanzania pia tuna Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo inataja haki za msingi za mtoto kama zilivyoelezewa kwenye mikataba hiyo na kueleza wazi kwamba katika kufanya maamuzi yoyote kuhusu mtoto kanuni ya maslahi bora ya mtoto lazima izingatiwe.


Mikataba hii na sheria ya mtoto inatoa wajibu kwa serikali, wazazi, walezi na wanajamii kwa ujumla kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili na ubaguzi.


Mfano katika mwaka 2021, masuala makuu yaliyoathiri haki za watoto kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi ni pamoja na ukatili wa kingono; ukatili wa kimwili na kisakolojia, ajira kwa watoto na utumikishwaji wa watoto, usafirishaji haramu wa watoto,ndoa za utotoni na mimba za utotoni.


Takwimu hizo za polisi zilionesha matukio ya ukatili dhidi ya watoto yalipungua kutoka matukio 15,870 mwaka 2020 hadi matukio 11,499 kwa mwaka 2021, sawa na punguzo la asilimia 27.5 lakini bado asilimia 85 ya waathirika wa matukio hayo 11,499 walikuwa ni watoto wa kike huku asilimia 15 iliyobaki wakiwa watoto wa kiume.


Vilevile takwimu ambazo zimewahi kutolewa na Shirika la Nukta Tanzania zinaonesha asilimia 22.8 ya wanawake hapa nchini waliolewa wakiwa hawajafikisha umri wa miaka 18 huku asilimia 37.2 ya wanawake waliolewa chini ya umri huo hawakuwahi kupata elimu rasmi.


Ni wazi kwamba bado jamii ina safari ndefu katika kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia hapa nchini ili kuwezesha kila mtu kuishi maisha ya amani na furaha kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo hapa nchini hivyo ni vizuri kila mtanzania mpenda amani akawa ni askari katika mapambano haya.


Matukio ya hivi karibuni katika mikoa ya Shinyanga ambako Mkuu wa Mkoa huo alilazimika kuvunja ndoa ya mwanafunzi wa kidato cha tano iliyokuwa ikifungishwa katika Kata ya Mwawaza na kule mkoani Ruvuma wazazi waliokuwa wakimuozesha mtoto wao kwa mahari ya shilingi 30,000 ni ushahidi tosha kwamba bado jamii haijakubali kubadilika.


Mkurugenzi wa Shirika la Agape la mkoani Shinyanga linaloshughulika na utetezi wa Haki za wanawake na watoto,John Myola anasema hali ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika Mkoa huo bado vipo hasa kwa upande wa watoto wa kike.
Myola ambaye kituo chake kinachowaendeleza kielimu waathirika wa mimba na ndoa za utotoni mpaka hivi sasa kina watoto wa kike wapatao 57 anasema changamoto ya mimba na ndoa za utotoni kwa Mkoa wa Shinyanga bado inahitajika juhudi za makusudi katika kukabiliana nayo huku akiiomba Serikali pia kuweka mkono wake badala ya maneno matupu.


Anasema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinahitaji vita kubwa kuvikomesha na kwamba Serikali sasa iangalie uwezekano wa kuzipatia ruzuku asasi zisizokuwa za kiserikali (NGO’s) zinazojishughulisha na upigaji vita vitendo vya ukatili hapa nchini.


“Imefika wakati sasa serikali ijikite kwa vitendo katika vita hii, maana mara nyingi wao wamekuwa wasemaji na wakemeaji tu lakini hakuna hatua za makusudi wanazochukua, sasa ioneshe kwa vitendo ushiriki wake katika vita hii, hasa kwa kutenga fungu la fedha kuzisaidia NGO’s zinazojishughulisha na kupinga vitendo hivi vya ukatili,”anasema na kuongeza kuwa


“Pili jamii iendelee kupatiwa elimu kuhusu madhara ya vitendo vya ukatili hasa kwa wanawake na watoto hii itasaidia katika kupunguza kama siyo kukomesha kabisa vitendo hivyo hapa nchini, tukishikamana vitendo vya ukatili itabaki kuwa historia katika nchi yetu,” anaeleza Myola.


Hata hivyo Myola anaishauri serikali iangalie upya sheria za makosa ya jinai na kanuni za adhabu zilizopo ili kuzifanyia marekebisho na kuwezesha watuhumiwa wa makosa ya ubakaji wasiwe wanapewa dhamana kwa lengo la kuzuia wasitoroke au kuharibu ushahidi mpaka pale watakapokuwa wamefikishwa mahakamani na kesi zao kusikilizwa na kutolewa hukumu.


Mkakati mwingine ni serikali iendelee kuweka msukumo katika suala la kuielimisha jamii juu ya madhara yanayowapata watendwa wa vitendo vya ukatili ili ielewe na iweze kuchukua hatua za makusudi katika kuvipiga vita, maana licha ya kila mwaka kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kasi ya kupungua kwa vitendo hivyo bado ni ndogo.


Katika kukabiliana na vitendo hivi vya ukatili hapa nchini waandishi wa habari kutoka mikoa 10 ya Tanzania wameanzisha Mtandao wa Kupiga Vita na Kupambana na vitendo vya Ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini unaofahamika kwa jina la Tanzania Journalist Against Violence & Gender (TAJOGEV).


Malengo makuu ya mtandao huu ni kutaka kuhakikisha jamii hapa nchini inabadilika na kuwachana na mila na desturi kandamizi na zilizopitwa na wakati na iwe na elimu ya kutosha kuhusu madhara makubwa yanayompata mtu anapotendewa kitendo chochote cha ukatili hasa upande wa wanawake na watoto.


Mwenyekiti wa TAJOGEV, Stella Ibengwe anasema waandishi wa habari ambao ni wanachama wa mtandao huo wanaamini iwapo wataungana pamoja katika kupaza sauti kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia kuna uwezekano mkubwa wa vitendo hivyo kupungua kama siyo kumalizika kabisa hapa nchini.


Mratibu wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mkoani Shinyanga, Glory Mbia mbali ya kuwapongeza waandishi kwa hatua waliochukua ya kuanzisha mtandao wa kupiga vita vitendo vya ukatili anawataka wanahabari kuhakikisha wanaandika habari zitakazoleta mabadiliko makubwa katika kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini.


“Niwapongeze sana kwa hatua yenu ya kuanzisha mtandao huu wa TAJOGEV, ni jambo jema sana, naamini kupitia kalamu zenu mtawezesha kusambaza maeneo mengi elimu kwa jamii ya kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini cha kuwaahidi ni ushirikiano wetu pindi mkiuhitaji,” anaeleza Mbia.


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi amesema maeneo mengi nchini hapa bado yanakabiliwa na vitendo vya ukatili hasa kwa wanawake na watoto na kwamba kupitia mtandao wa TAJOGEV anaamini vitendo hivyo vinaweza kupungua kama siyo kumalizika kabisa.


“Niwashukuru kwa kuliona hili tatizo na mkaamua kuanzisha mtandao huu ni jambo jema, kikubwa ninachowaomba wakati mkipiga vita ukatili dhidi ya wanawake na watoto pia tupieni macho upande wa wanaume, wapo wanaofanyiwa ukatili na wenza wao,”anasema na kuongeza kuwa


“Wapo wanaume wanaokutana na matatizo mengi, wanafanyiwa ukatili lakini wanavumilia kwa sababu wanaona aibu iwapo watatoa taarifa za ukatili wanaotendewa nyumbani na mara nyingi wengi wao hujikuta wakiathirika kisaikolojia, sasa pazeni sauti pia ili waweze kutoa taarifa juu ya ukatili uliopo ndani a familia zao,” anaeleza Samizi.