Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Korogwe
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Halfan Magani amewataka Wasimamizi Wasaidizi wa vituo vya kupiga kura kwenye Uchaguzi mdogo wa Kata ya Kwashemshi kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.
Amesema moja ya kazi yao ni kuhahakisha hawaleti taharuki kwenye uchaguzi huo, na kusema mgombea atakaeshinda basi ashinde kwa halali.
Ameyasema hayo Julai 10, 2023 wakati anafungua mafunzo ya siku mbili kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi na Makarani waongozaji wapiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Kwashemshi Wilaya ya Korogwe.
Magani amesema washiriki wa zoezi hilo wamekula kiapo ili kufanya kazi hiyo ya kusimamia zoezi la upigaji kura.
Ni matumaini yake wote watafanya kazi hiyo kwa uadilifu na uaminifu, na bahati nzuri karibu asilimia 99.9 wameshiriki shughuli kama hiyo siku za nyuma, hivyo yeyote atakaejaribu kuharibu, watamuweka pembeni.
“Zoezi hili ukiharibu kidogo madhara yake ni makubwa,kunahitajika umakini mkubwa Kwenye hili zoezi tukiona unataka kutuharibia tunakuweka pembeni,mmekula kiapo ili kutunza siri, na kama huna uwezo wa kutunza siri, tueleze tukuweke pembeni, usije ukasababisha uchaguzi kurudiwa”
“Tunataka mfanye kazi kwa ushirikiano ili kuona zoezi hili linakwenda vizuri. Usije ukaharibu, maana kosa moja ukilifanya, uchaguzi wote unaweza kurudiwa. Hivyo tunataka ufanye kazi hii bila kuleta taharuki kwenye jamii, na atakaeshinda ashinde kwa halali,”amesema Magani.
Magani amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwataka wajue wajibu wao kama Makarani waongozaji wapiga kura na taratibu za uchaguzi, hivyo ni matumaini yake baada ya mafunzo hayo kila mmoja ataelewa majukumu yake, na kufanikisha uchaguzi huo.
Akizungumza nje ya mafunzo hayo ya siku mbili, Ofisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Samina Gullam amesema uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kwashemshi (CHADEMA) Twahiru Tindikai kujihudhuru na kutimkia CCM.
CCM imempa nafasi nyingine Tindikai, ambapo yeye ndiyo atapeperusha bendera ya chama hicho
Wagombea watano wameingia kwenye kinyang’anyiro hicho, ambapo uchaguzi huo utafanyika Julai 13, 2023 siku ya Alhamisi ambao ni Said Ngoma wa ADC, Majaliwa Kipepe wa ACT- Wazalendo, Hozza Hozza wa DP, na Juma Gao kwa tiketi ya ADA TADEA
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa