Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini RITA, yasajili vyeti vya kuzaliwa ndani ya siku moja katika maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa, Dar es Salaam (Saba Saba) yanayoendelea hadi hivi sasa.
RITA imesajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa papo hapo kwenye maadhimisho ya Saba Saba yaliyofanyika mwishoni mwa wiki ambapo kwa siku hiyo tu walitoa jumla ya vyeti vya kuzaliwa 250 ambapo mpaka sasa wanaendelea kutoa mpaka Julai 13,2023.
Akiwakabidhi vyeti vyao vya kuzaliwa wananchi waliojitokeza kujisajili kwenye sikukuu hiyo ya Sabasaba, Naibu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA, Irene Lesulie, amesema RITA imejipanga vizuri kuwapatia huduma wananchi kiurahisi na kuwataka kutumia fursa hii kujitokeza kwa wingi ili waweze kupatiwa huduma kwenye maonesho hayo yanayotarajiwa kumalizika Julai 13, Mwaka huu.
“Nawasihi wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi wasiache fursa hii iwapite kwenye maonesho haya ya saba saba, tunasajili na kutoa vyeti hapa hapa katika banda letu,”amesema Lesulie.
Aidha, baadhi ya wananchi waliojitokeza kusajiliwa na kufanikiwa kupata cheti kwenye viwanja hivyo vya sabasaba wameipongeza RITA kwa kuwarahisishia huduma ya kuwapatia vyeti kwa siku moja.
“RITA wako vizuri kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa hapa hapa sio mchezo,kwa watu tulivyojaa sikutegemea kupata cheti leo”, amesema Salma Ubuguyu, ambaye ni mmoja wa wananchi waliojitokeza kwenye banda la RITA na kupatiwa cheti cha kuzaliwa papo hapo.
RITA inaendela kutoa huduma ya usajili wa vyeti vya kuzaliwa,elimu ya mirathi kuandika na kuhifadhi wosia kwenye maonesho hayo hadi tarehe 13 Julai 2023 .
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa