January 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashindano ya Gofu kufanyika sabasaba

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MASHINDANO makubwa na ya kipekee ya gofu kwa watoto na watu wazima, yanatarajiwa kufanyika Julai 7, 2023 (Saba Saba Day) katika viwanja vya mchezo huo vya Gymkhana, jijini Dar es Salaam, yakidhaminiwa na Lake Energy Group.Lake Energy Group wanajishughulisha na uuzaji na usambazaji wa petrol, dezeli, gesi, mafuta vilainishi ya mashine, nondo na bidha nyinginezo pamoja na kutoa huduma ua usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Julai 2, 2023, Mkuu wa Mauzo wa Lake Energy Group, Stephen Munguti, alisema kuwa watatoa zawadi kwa washindi wa mashindano hayo ambayo lengo lake ni kuisapoti Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto na watu wazima katika michezo.

Alisema kuwa wakifahamu kuwa michezo ni ajira inayolipa kama zilivyo nyingine, wanaamini kupitia mashindano hayo, wataibua vipaji vitakavyotamba baadaye katika klabu mbalimbali na hatimaye kuipeperusha vema Bendera ya Tanzania kimataifa.

“Lake Energy Group tumeona ni vema tukaungana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kupromoti michezo na wanamichezo.

“Tunafahamu pamoja na masomo, watoto wanatakiwa pia kujengwa kimwili na kiafya kiujumla, hivyo kupitia mashindano haya, watoto wetu watakuwa wameimarika kiafya na kujenga tabia ya kushiriki katika michezo mara kwa mara kama itakavyokuwa kwa washiriki wengine,” alisema,Munguti

Kwa upande wake, mwandaaji wa mashindano hayo, Fredrick Laiser, alisema kuwa wamefanya hivyo ili kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto na watu wazima katika mchezo huo maarufu duniani.

Aliwashukuru Lake Energy Group kwa kukubali kudhamini mashindano hayo, huku akiwataka wadau zaidi kujitokeza kuwasapoti ili kuzidi kuyanogesha mashindano hayo katika siku za usoni.

“Tunawaalika wazazi na walezi wa watoto watakaoshiriki na wadau wa mchezo wa gofu na wanamichezo kwa ujumla, kujitokeza kwa wingi pale Gymkhana Club, Dar es Salaam kushuhudia vipaji katika mchezo wa gofu,” alisema Laiser.M