November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe

Kenya kupima watu wote walioingia nchini humo

NAIROBI, Wizara ya Afya nchini Kenya imeanza kufanya upimaji wa virusi vya corona (COVID-19) kwa watu wote walioingia nchini humo wiki iliyopita. Sambamba na wale waliowekwa karantini kwenye vituo vya serikali au hoteli zilizoteuliwa.

Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe alisema, upimaji huo utafanyika kwa mujibu wa miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu upimaji wa corona, na kulingana na tarehe ya kuwasili kwao.

Kagwe pia alisema,kutokana na hatari ya corona, na shinikizo kubwa kwa rasilimali za huduma za afya, ni muhimu kwa serikali kuwalazimisha watu waliothibitika na wale waliokaribiana nao kuwekwa kwenye karantini.

Aidha, aliwataka Wakenya kuzingatia usafi binafsi kwani ni msingi wa kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. Hadi sasa watu 42 wameambukizwa corona nchini Kenya huku mtu mmoja akifariki na mwingine akipata nafuu. Wakati huo huo hadi sasa Serikali ya Kenya imewapima watu 1,141 na miongoni mwao 163 wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya karantini ya siku 14 huku wengine 978 wakiendelea kufanyiwa uchunguzi baada ya kukutana na watu waliokuwa na corona.