December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vibari vya kuingiza mifugo mipya Kalambo vyasitishwa

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa

Mkuu wa wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa Lazaro Komba amemwagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmshauri ya Kalambo kusitisha utolewaji wa vibari vya kuingiza mifugo katika kijiji cha Madibila kutokana kijiji hicho kuwa na mgogoro kati ya wafugaji na wakulima uliosababisha baadhi wafugaji kupigwa na kuumizwa kutokana na kulisha na kupitisha mifugo kwenye mazao ya wakulima.

Ameyasema hayo kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mabidila wilayani humo na kusisitiza kila mfugaji kutumia eneo lake katika kulisha mifugo yake .

Alisema kuwa mfugaji ni lazima aitathimini idadi ya mifugo aliyonayo ukilinganisha na eneo lake la malisho alilonalo na kuwa kwa kufanya hivyo watapunguza migogoro kati yao na wakulima.

Mkuu huyo wa wilaya alitaka halmashauri sasa kutengeneza utaratibu mzuri kupitia serikali za vijiji kutopokea mifugo mipya toka kwa wafugaji kama watakua hawana maeneo ya kutosha ya kuchungia.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Kalambo Nicholaus Mlango aliunga mkono kauli hiyo ya mkuu wa wilaya na kuviagiza vijiji vyote ikiwemo cha Madibila kutopokea tena mifugo mipya na kutaka agizo hilo kutekelezeka.

Alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha amani ili waweze kufanya shughuli zao vizuri na kukuza uchumi na ndiyo maana hawataki migogoro itokee kati ya Wafugaji na Wakulima.

Mmoja kati ya Wananchi ambaye ni mkulima Sande Sichilima alidai kuwa kama agizo hilo la serikali la kusitisha vibali vya kuingiza mifugo katika vijiji litatekelezeka imani yake ni kuwa migogoro itatoweka kabisa.

Alisema kuwa katika kijiji hicho cha Madibira mifugo imekuwa mingi ukilinganisha na eneo la malisho na ndiyo maana migogoro imeanza kujitokeza na kuishukuru serikali kwa hatua hiyo iliyoichukua ya kusitisha vibali vipya vya kuingiza mifugo katika wilaya hiyo.

Ntinga Luhende ambaye ni mmoja wa Wafugaji alidai kuwa wao wamepokea maamuzi ya serikali na watahakikisha mifugo mipya aipelekwi katika wilaya ya Kalambo hususani kijiji cha Madibira.

Mkuu wa wilaya Kalambo Razaro Komba akizungumza na Wananchi wa Madibira juu ya kuondoa kero za migogoro ya Wakulima na Wafugaji