December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATCL kuongeza ndege tatu za abiria

Na Penina Malundo,Dar es Salaam

SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) limesema kuwa hivi karibuni linatarajia kuongeza ndege nyingine tatu za abiri ikiwemo ya aina ya Boeing 737 MAX 9 na moja ya masafa marefu aina ya Dreamliner.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo katika maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam alisema hali ya Shirika inaendelea kuimarika siku hadi siku na kuendelea kuongeza idadi ya ndege.

Alisema mpaka sasa idadi ya ndege zilizopo ni 12 huku tunatarajia kuongeza ndege nyingine Tatu ikiwemo Dreamliner Moja ambayo itafanya kwa jumla ya ndege tatu aina ya Dreamliner.

“Tulikuwa na changamoto ambayo sio ya ATCL pekee ni ya dunia nzima kuhusiana na ndege za Airbus lakini sasa hivi tuna uhakika kufikia katikati au mwisho wa mwezi huu ndege mbili zitakuwa zimerudi kwahiyo tutakuwa na ndege tatu za Airbus na ya nne tunategemea kufikia mwishoni mwa mwezi wa nane au tisa ndege zote zitakuwa kwenye kutoa huduma,” amesema Matindi.

Amesema hiyo inatokana na sasa waundaji wa injini ambazo ndo zilikuwa na tatizo wameweza kujipanga hasa kukabiliana na changamoto hiyo.

“Hii ni habari nzuri kwamba nguvu yetu ya kufanya biashara itaongezeka. Tunajua tuna mahitaji makubwa kwa sasa ikiwemo katika Mkoa wa Mwanza ambapo ndege zinazoenda hazijitoshelezi,” amesema.

Akizungumzia uwanja wa ndege wa Dodoma,Matindi amesema kuna juhudi kubwa zinazofanywa na serikali za kuongeza taa katika uwanja wa ndege wa dodoma ili ndege ziweze kutua usiku.

Amesema zoezi hili linaendelea na kufikia kati ya mwezi wa tisa hadi wa 11 utakuwa umekamilika ipasavyo na kuwa tayari kwa kutua ndege wakati wote.

Hata hivyo amesema kuwa wanatarajia kupokea ndege mpya ya mizigo na tayari wameshamaliza taratibu zote na mafunzo ya marubani pamoja na usajili.

“Sehemu kubwa ambazo tunatarajia kufanya biashara ikiwemo Mumbai, India, Lubumbashi, Lusaka, Zimbabwe, Entebbe na Kinshasa. Pia tutaongeza na sehemu zingine…kwahiyo ndugu zangu ATCL sio abiria tu, itakuwa suluhisho kwa wafanyabiashara,” amesema Matindi.