December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waleeni yatima kwa wema mpate baraka-Sheikhe Kabeke

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

SHEIKHE wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke, ameitaka jamii na waumini wa Dini ya Kiislamu kurudisha imani,kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuwalea yatima na kuwatendea kwa wema ili adhabu siku ya kiama wawe bega kwa bega na Mtume Muhhamad S.A.W.

Pia amesema Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) la sasa likiwemo la Mkoa wa Mwanza akilipima kwa miaka mitano iliyopita kuna mabadiliko makubwa kwani mengi yamefanyika na kuondoa sura ya kutokuaminika kwenye jamii wakiwemo waislamu.

Watoto yatima kutoka vituo mbalimbali vya dini ya kiislamu pamoja na Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke (wa pili kutoka kulia) wakishiriki kula chakula cha mchana kilichoandaliwa na BAKWATA hapa kwa hisani ya Mkurugenzi wa kampuni ya The Rocky Solution, Zakaria Nzuki.

Ametoa kauli hiyo leo wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa na BAKWATA Mkoa wa Mwanza, kwa hisani ya Mkurugenzi wa Kampunua ya The Rocky Solution Ltd, Zakaria Nzuki, ukiwa ni mwendelezo wa sherehe ya Ibada ya Eid El Adhaa.

Sheikhe Kabeke amesema waislamu wanao wajibu wa kurejesha imani,kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuwalea yatima katika nyumba zao na kuwatendea kwa wema waondokane na huzuni ya kuwapoteza wazazi wao wawaone ninyi ndio baba na mama,kufanya hivyo siku ya kiama watakuwa bega kwa bega na Mtume S.A.W kwa saba

“Mpinga dini ni yule asiyewajali yatima,tunavyoona nyota ziking’aa angani ndiyo Malaika Mbinguni wanaona duniani nyumba (si nyota) kuwa ile ni nyumba anaishi yatima.Turudishe imani na kuwajali yatima tuishi nao katika nyumba zetu,tusiwageuze watumishi wa ndani,tuwatendee kwa haki na wema,”amesema.

Sheikhe huyo wa mkoa amesema waislamu wakiimarisha utamaduni wa kuwalea yatima watapata baraka kwa sababu katika pepo kuna nyumba ya furaha ambayo wanaoingia humo ni walioishi na kuwajali yatima na kuhoji laiti kila mtu angechukua yatima mmoja vituo vilivyojengwa vya kulea vingetoka wapi?

Amemshukuru Nzuki kwa kutoa sadaka ya chakula kwa watoto yatima kwa zaidi ya miaka mitatu ingawa si mwislamu ambapo baadhi ya waislamu na wasio waislamu wameanza kuiga mfano huku akiwashukuru waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kusaidia BAKWATA kutangaza kazi zake na kuhakikisha zinawafikia wananchi.

Pia amemshukuru Mufti Sheikhe Mkuu, Abubakar Zuberi Mbwana Bin Ali kwa kuibadilisha BAKWATA kwa kiwango kikubwa,ibada zote zimerejeshwa na zinaendeshwa kwa taratibu na imani ya kiislamu na mengi ya jamii ya kiislamu na kijamii.

Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke,akizunguma na watoto yatima wanaolelewa katika vituo mbalimbali vilivyo chini ya BAKWATA mkoani humu, leo kabla ya kushriki kula nao chakula cha mchana.

“Tunamshukuru Mufti,ameshiriki kuchimba visima,ujenzi wa vituo vya afya na mengine mengi.Tunajitahidi kufuta tuhuma na propaganda chafu dhidi ya BAKWATA sasa inaaminika kwa jamii na waislamu tofauti na miaka mitano iliyopita,”amesema Sheikhe Kabeke.

Naye Kadhi wa Mkoa wa Mwanza, Sheikhe Hamis Almasi amesema Mwenyezi Mungu ana watu wenye busara sana na kuwataka waislamu wafanye kazi ya kumtafuta, bila kuwajali yatima dunia itawachukulia mambo mengi kwani wanaoangalia mambo ya Mungu wameipa talaka wakabaki kuangalia ya Mungu.

Awali mwanafunzi Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Thaqaafa, Husein Yusuph amewaliwaonya waislamu kutowadhulumu yatima mali zao kwa kuwalaghai wanawatunzia kuwa watakumbana na moto.

Alisema wawaenzi na kuwatunza yatima ili wasiwakumbuke wazazi wao lakini wakiwatendea kinyume kwa kuwanyanyasa na kuwatenga kutawafanya wawakumbuke wazazi wao.

“Mwenyezi Mungu anasema wanaopinga dini ni wanao wanyanyapaa na kuwadhulumu yatima mali zao, humlipa akila anayegusa nywele na kichwa cha yatima na nyumba bora ni anayoishi yatima na kupewa haki zake na nyumba mbaya ni aishiyo yatima lakini hapewi stahiki zake,”amesema Yusuph.

Aidha katika hatua nyingine Sheikhe Kabeke amewahimiza mshikamano na kuishi kwa amani na utulivu, kila Matanzania aitunze amani iendelee kudumu pamoja na kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema Rais Samia anapaswa kuombewa utamduni ambao umeendelea kwa Marais wote wa nchi hii, pia anafanya mambo makubwa licha ya kuipokea nchi katika kipindi kigumu cha majonzi baada ya mtangulizi wake kufariki dunia.

“Alipokea nchi kwenye kipindi kigumu lakini inakwenda,miradi aliyoibeba inaendelea mwingine angeweza kuiacha akaanzisha ya kwake,tumwombee Rais wetu Mwenyezi Mungu amlinde na kumwepusha watu wabaya wenye nia ovu, chuki na husuda,”amesema.

Ameshauri waislamu baada ya ibada katika hotuba zao misikitini wawe na utamaduni wa kuzungumza mambo yanayotokea kwenye jamii,wafanye kwa uwazi na kukemea mabaya na yenye athari kwa nchi.