November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WCF yaadhimisha Siku ya Utumishi wa Umma kwa kutoa msaada Hosptitali ya Mwananyamala

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID. 

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umekabidhi vifaa tiba kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo huadhimishwa Juni 23 kila mwaka kwania ya kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika Maendeleo ya bara la Afrika. 

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge alisema

Hospitali na watoa huduma za afya ni wadau muhimu nan i kiungo baina ya Mfuko na wahanga wanaopata magonjwa au ajali zinazotokana na kazi na jukumu kubwa la WCF ni kutoa fidia pale mfanyakazi anapoumia au kuugua kutokana na kazi hivyo msaada huo ni kutambua mchango wa watumishi wa umma katika kuhudumia wananchi na Mfuko unaamini msaada huo utarahisisha utendaji wao wa kazi na hivyo kuleta tija katika sekta ya afya. 

“Watumishi ni sehemu ya umma na WCF ni sehemu ya umma kwa sababu inatoa fidia kwa wafanyakazi, na ninyi mnahudumia jamii, tunajua mnatoa huduma nzuri, lakini tukiwaunga mkono kwa kutoa vifaa zaidi mtatoa huduma zenu kwa ubora zaidi na wagonjwa mnaowahudumia watapona haraka na kurejea katika uzalishaji na hivyo kujenga uchumi wa taifa.” Alifafanua. 

Bi. Laura aliipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha huduma za afya nchini ambapo inashuhudiwa ongezeko kubwa la miundombinu ya afya katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Katibu wa Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, Bi. Lydia Nzema aliishukuru WCF kwa msaada huo wa vifaa tiba ambavyo alisema vitasaidia kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi. 

“Hospitali hii ni ya umma inahudumia jamii yote iliyo katika eneo hili, na tunahudumia watu wengi vifaa hivi vitarahisisha na kupanua wigo wa wagonjwa tunaowahudumia kwani uhitaji ni mkubwa sana.” Alifafanua.

Aidha kwa upande wao Maafisa Wafawidhi Kanda, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kutoka Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini na Kanda wa ziwa, wametoa wito kwa waajiri kujisajili na Mfuko ili kuwawezesha watumishi wao kuwa na uhakika wa kipato pindi wanapopatwa na majanga wawapo kazini. 

“Tunapenda kuwakumbusha watumishi wa umma Tanzania bara kuzingatia miongozo ya usalama na afya amahli pa kazi, lakini inapotokea bahati mbaya mtumishi amepata changamoto ya ajali kazini au ugonjwa afike ofisi za WCF ili aweze kupata hakiz ake kama mtumishi.” Alisema Nuru Ashraf, Afisa Mfawidhi WCF, Kanda ya Kati.

Naye Rose Satta, Afisa Mfawidhi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, alisema katika maadhimisho hayo wameendelea kutoa elimu na kuwahudumia waajiri na watumishi mbapo alisema Mfuko umerahisisha sana utoaji wa huduma kwa njia ya kidijitali hivyo watumie huduma hiyo kutoa taarifa za matukio ya ajali, magonjwa au kifo kwani itarahisisha Mfuko kuchataka madai yao kwa haraka.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge (mwenye miwani) akimkabidhi vifaa hivyo Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Bi. Lydia Nzema.

Baadhi ya Wafanyakazi wa WCF na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala wakiwa katika picha pamoja na vifaa hivyo. 

Afisa Mfawidhi WCF Kanda ya Kati, Bi. Nuru Ashraf (kulia) akimkaribisha ofisini kwake mtumishi wa umma, Bw. Juma Kengele ili kumuhudumia Juni 23, 2023.
 Afisa Mfawidhi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi. Rose Satta (kushoto) akimuhudumia mteja kwenye ofisi za WCF, jijini Mbeya.


Afisa Mfawidhi WCF, Kanda ya Ziwa, Bw. Said Ismail (kulia) akizunhgumza na watumishi wenzake Juni 23, 2023.

Mtumishi akihudumiwa na Afisa wa WCF ofisi ya Arusha Juni 23, 2023.