November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Madini yaanika vipaumbele 2023/24

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online MWANZA

MAAFISA Habari kutoka Vitengo vya Mawasiliano Serikalini vya wizara wameshiriki katika mafunzo ya kuhuisha taarifa za Wizara na Taasisi zilizo chini yake katika Tovuti Kuu ya Serikali yaliyoanza juni 22 hadi juni 24, 2023 jijini Mwanza.

Vipaumbele vya Wizara ya Madini Mwaka wa Fedha 2023/24 vilivyohuishwa kwenye Tovuti Kuu ya Serikali ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, Kuendeleza madini muhimu na madini mkakati, kuwaendeleza na kusogeza huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo.

Vile vile, kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini, kuhamasisha uwekezaji na biashara katika Sekta ya Madini, uanzishwaji wa minada na maonesho ya madini ya vito.

Pia, kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Idara ya Habari-MAELEZO kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha taarifa zote muhimu za Wizara na Taasisi zake zikiwemo huduma zinazotolewa kwa njia ya mtandao zinapatikana katika tovuti hiyo ili kuwarahisishia wahitaji wa huduma hizo ndani na nje ya Tanzania kupata huduma hizo kwa urahisi.