Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga
TAASISI ya Mzalendo Foundation yenye makazi yake wilayani Kahama Mkoani Shinyanga imeunga mkono hatua za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la ubinafsishaji wa bandari ya Dar es Salaam.
Katika tamko lake kwa waandishi wa habari mkoani Shinyanga Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Khamis Mgeja amesema baada ya kufanya utafiti wa kina wamebaini serikali imezingatia maslahi yote ya nchi katika ubinafsishaji wa bandari hiyo ya Dar es Salaam.
Mgeja amesema wamefanya uchambuzi wa kina pamoja na kufuatilia mijadala mbalimbali ikiwemo kusikiliza Bunge, na wamejiridhisha pasipo shaka yoyote, kwamba mpango wa Serikali kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar-es-Salaam ni mzuri na wameunga mkono asilimia 100 kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Sisi kwa upande wetu tumejiridhisha kabisa kuhusu sakata hili la uwekezaji wa bandari yetu, kupitia uchambuzi wa kina pamoja na kufuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa ikiendelea bungeni, tumeridhika na hatuna shaka kabisa kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali yetu kwenye suala hili,”amesema Mgeja na kuongeza kuwa
“Niseme ukweli kabisa sisi tuna imani na Serikali na haiwezi hata siku moja kupotosha umma wa kuuza maslahi ya nchi, tumeona Bunge letu limeridhia suala hili, na sisi kama watanzania, tunasimama kifua mbele kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan juu ya uwekezaji wa bandari yetu baina ya Tanzania na mwekezaji kutoka Dubai,” ameeleza Mgeja.
Amesema baada ya kujiridhisha yeye na Taasisi yake wanaunga mkono kwa asilimia 100 ubinafsishaji wa bandari kwa maslahi mapana ya Taifa na kwamba wale wote wanaopinga hatua hiyo ni wazi hawaitakii mema nchi ya Tanzania na wanataka irudi nyuma katika kupiga hatua kwenye maendeleo.
Amesema kuna mambo ambayo yamekuwa yakimkera kupitia mitandao ya kijamii hivyo ameamua kuyazungumza ili kuyaweka sawa hasa upande wa wanaopotosha wakipandikiza chuki kwenye masuala ya udini na ukabila ambayo hayana afya yananayoweza kuligawa Taifa.
“Niwaombe watanzania wazipuuze propaganda zote zinazosambazwa kwa nguvu kupitia mitandao ya kijamii na wanasiasa ambao hawataki kuiona Tanzania ikipiga hatua za haraka katika maendeleo na badala yake waungane kuunga mkono maamuzi ya Serikali badala ya kuyapinga,”
Pia maesema suala la ubinafsishaji katika nchi yetu halijaanza katika awamu ya sita, limeanza kitambo tangu enzi za Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, sasa hakuna sababu ya kutaka kuupotosha umma eti serikali ya awamu ya sita imeamua kuuza nchi.
“Siyo kweli kabisa, nishauri tu inapotokea eneo halina ufanisi, ni vyema wakatafutwa wawekezaji ili kuongeza ufanisi,namuomba Rais Samia azibe masikio na akaze mkanda katika kuwatumikia watanzania ili Tanzania iweze kupiga hatua za haraka kwenda kwenye maendeleo,”amesema.
Aidha amesema kuwa wapotoshaji hawajaanza leo bali hata huko nyuma walikuwa wakipinga mambo mengi yenye maslahi kwa taifa mfano wa suala la kutangaza utalii kupitia filamu ya Royal Tours ambayo kwa sasa matokeo yake yanaonekana.
“Ni wazi kuwa bandari yetu ilikuwa haituingizii kipato stahiki, sasa huyu mwekezaji yeye ameonesha wazi ataiboresha na Taifa letu tutapata mapato makubwa ambayo yatasaidia kusukuma kwa haraka miradi yetu mbalimbali ya kimkakati, tuwaombe wapotoshaji waache,” ameeleza Mgeja.
Mgeja ameonya wanaopinga uwekezaji ambao umefanyika waache kuhusisha suala hilo na udini, ukabila au ukanda, na ikiwezekana waeleze wao wanataka mwekezaji awe ni mtu mwenye dini au kabila ipi?.
Huku akisisitiza waache upotoshaji na badala yake waje na mawazo ya kujenga nchi na siyo kuwajaza chuki watanzania.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa