November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Barabara za EPC + F hazitalipiwa

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Serikali imesema kuwa utekelezaji wa miradi saba ya ujenzi wa barabara kwa njia ya EPC+ F haitalipiwa na wananchi watakaotumia barabara hizo kama ambavyo baadhi ya wananchi wanavyodhani.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, wakati wa utiaji saini wa miradi hiyo ambayo inatarajiwa kutekelezwa katika Kanda za Kaskazini na Kusini na kujengwa na makandarasi wanne (4).

“Tanzania haina barabara za kulipia mpaka sasa, hivyo upotoshaji unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kulipia kwenye barabara hizi si sahihi kwani barabara hizi ni za kawaida ‘high way’ kama zilivyo barabara nyingine” amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa mradi huu ni wa kwanza na mkubwa kutekelezwa nchini kwani utapita katika mikoa 13 na lengo likiwa ni kuboresha mtandao wa barabara nchini na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji ili kuchochea uzalishaji katika maeneo zinapopita barabara hizi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Barabara zitazojengwa zitapita katika mikoa ya Morogoro, Ruvuma, Arusha, Manyara, Dodoma, Tanga, Singida, Mbeya, Songwe, Lindi, Mtwara, Simiyu na Iringa na hivyo zitarahisisha usafiri wa wananchi na usafirishaji wa mazao ya misitu, biashara, chakula, uvuvi na ufugaji, malighafi za madini kama vile makaa ya mawe, grafaiti na Chuma”, amefafanua Waziri Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa ametaja miradi itakayotekelezwa kuwa ni ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Kilosa Mpepo – Londo – Lumecha/Songea (km 435.8) , Barabara ya Arusha – Kibaya – Kongwa (km 453.42), Handeni – Kiberashi – Kijingu – Njoro – Olboroti Mrijo Chini – Dalai – Chambalo – Chemba – Kwa Mtoro – Singida (km 384.33), Igawa – Songwe – Tunduma (km 237.9), Masasi – Nachingwea – Liwale (km 175), Karatu – Mbulu – Hydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (km 339) na barabara ya Mafinga – Mtwango – Mgololo (km 81).

“Katika ujenzi wa barabara ya Igawa – Tunduma mkoani Mbeya Serikali imeamua kuijenga kwa njia nne ambapo barabara moja kati ya hizo itatumiwa na wasafirishaji wa malori tu ili kupunguza msongamano wa magari uliopo sasa katika eneo la Tunduma”, amefafanua Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amebainisha faida nyingine ya utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo kuchochea kiu ya matumizi ya bandari zetu kwa nchi jirani za Zambia, Malawi, Zimbabwe, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani ya Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Pia ametaja kuwa barabara hizo zitatoa ajira za moja kwa moja kwa watanzania takriban 20,300 pamoja na kuwajengea uwezo wahitimu wa vyuo vikuu kwa masharti ya mikataba ya ujenzi na usimamizi ambapo wahitimu wasiopungua 70 watapata ajira.

Prof. Mbarawa ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kushirikiana na Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB) kuandaa wahandisi washauri wazawa watakaokuwa na uwezo na weledi wa kusimamia miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa nchini.

Awali akitoa taarifa ya miradi hiyo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta, ameeleza kuwa jumla ya makandarasi 129 walionesha nia ambapo mchakato wa zabuni ulipitia hatua mbalimbali na hatimaye makandarasi wanne walikidhi vigezo vilivyowekwa.

“Makandarasi watakuwa timu nne kwa kila mradi mkubwa ambapo sehemu zote zitaanza kutekelezwa sambamba kwa wakati mmoja ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hii” “amesisitiza Mha. Besta.

Ameongeza kuwa kupitia utaratibu huo makandarasi watawajibika kufanya usanifu wa kina na kujenga barabara hizo kwa viwango na ubora ulioainisha kwenye mkataba na huku vihatarishi vyote vinavyohusu usanifu wa mradi na muda wa ujenzi vitabebwa na mkandarasi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso, amesema kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania inaandika historia ya kujenga barabara (Km 2,035) kwa mara moja wakati hapo awali Serikali ilikuwa inajenga Kilometa 200 hadi 250 kwa mwaka.

Utiaji saini wa mikataba Saba ya miradi ya ujenzi wa Barabara umefanywa na Serikali kupitia TANROADS na Kampuni ya China Civil Engineering Construction (CCECC), Sinohudro Cooperation, China Overseas Engineering Group (COVEC) na China Railway 15th Group kwa gharama ya Trioni 3.7.