November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Batilda apongeza ufanisi Manispaa Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

HALMASHAURI ya manispaa Tabora imepongezwa kwa ufanisi mzuri wa kazi ambao umeiwezesha kupata hati safi kutokana na ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akihutubia kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika jana katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Alisema hati hiyo ni ishara ya umoja na mshikamano uliopo baina ya Ofisi ya Mkurugenzi, Wataalamu, Madiwani na Watendaji ikiwemo usimamizi thabiti wa fedha za miradi ya maendeleo inayotekelezaji katika halmashauri hiyo.

Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa halmashauri kuwajibika ipasavyo na kutojihusisha na vitendo vya ubadhirifu ambavyo hupelekea kupata hati yenye mashaka au mbaya.

‘Mtumishi yeyote anayebainika kusababisha hoja za ukaguzi zilizotajwa na CAG katika idara yoyote achukuliwe hatua stahiki za kisheria au za kinidhamu ili kuongeza umakini kwa watumishi wote’, alisema.

RC Batilda aliagiza Wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha ufungaji taarifa za hesabu zao za mwisho unandaliwa mapema na kuwasilishwa kwa mkaguzi wa ndani kabla ya kuwasilishwa kwa CAG kama Memorandam ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa  ya mwaka 2009, Kifungu Na. 14(4)(d) inavyoelekeza.

Aidha aliwataka kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa watumishi wote 

watakaosababisha uwepo wa hoja hizo na hesabu kutokaguliwa kabla ya kuwasilishwa kwa CAG.

‘Napenda kuchuka nafasi hii, kulikumbusha Baraza lako kuhakikisha linawachukulia hatua kali watumishi wote wanaosababisha hoja zinazoleta hasara pasipo upendeleo wala kumuonea Mtu yeyote’, alisema.

Aidha aliagiza Halmashauri hiyo kuihakikisha hoja zote zinapatiwa majibu stahiki na kuwasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu wa nje (CEA) kwa ajili ya uhakiki na kufungwa.

RC alionya kuwa bado kuna utekelezaji hafifu wa Maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa  (LAAC) kwani licha ya Halmashauri hiyo kupewa maagizo  31 kati ya mwaka 2013 hadi 2023, maagizo yaliyohakikiwa na kufungwa ni ishirini na tatu (23) huku (8) utekelezaji wake ukiwa bado unaendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Batilda Burian akiongea na madiwani wa halmashauri ya manispaa Tabora katika kikao maalumu cha kupitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) jana mjini hapa, kulia kwake ni Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa hiyo Ramadhan Kapela ambaye ni diwani wa kata ya Isevya. Picha na Allan Vicent.Â