December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dk. Mongella ataka gamba la Ushoga, usagaji livuliwe

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Getrude Mongella amesema vitendo vya mahusiano ya jinsia moja si jambo la kuachwa liendelee na kuitaka jamii kuvikemea kwani vinaharibu maadili ya Mtanzania.

Dk. Mongela aliyasema hayo jana wakati akizindua kitabu kijulikanacho kama ‘Jivue ngozi ya udhaifu’ kilichoandikwa na Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dorothea Simkwayi.

“Hatukupigania nchi hii watu waje kuuza vilainishi au kutengeneza vitabu vyenye kashfa, nchi hii hatukuikomboa ili watu waje wafanye mazagazaga yao, haiwezekani, msiturudishe nyuma…kama wapo waliofika hapo hilo ni gamba livuliwe,” alisema Dk. Mongela.

Aliwataka waandishi kuandika vitabu vitakavyolijenga taifa badala ya kuacha fursa hiyo kutumiwa na watu wengine wasioitakia mema Tanzania.

“Dorothea ametuonyesha katika umri mdogo ambao sisi wazee tumeshindwa kuandika vitabu, unatakiwa uonyeshe kile unachoweza kufanya kabla ya kusema fulani atafanya,” alisema.

Kuhusu kitabu hicho, Dorothea alisema kinamsaidia kijana kutambua kipawa alichonacho na kukitumia vema katika kuisaidia jamii inayomzunguka.

“Wazo la kuandika kitabu nililipata tangu nikiwa kidato cha tatu, nilipitia changamoto za kiafya na nikiwa hospitali nilianza kupata mawazo ya kuandika kitabu,” alisema Dorothea.

Kwa upande wake Mhariri na Mchapishaji wa kitabu hicho, Dk. Leonard Bakize, alisema kitabu hicho kinaakisi maisha aliyoyapitia Dorothea na kwamba kinafundisha watu kutokata tamaa.