November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NBC yazindua usajili mbio za NBC Dodoma Marathon 2023

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya NBC imetangaza kufanyika kwa mbio kubwa za NBC Dodoma Marathon mwaka 2023 siku ya Jumapili tarehe 23 Julai 2023 mkoani wa Dodoma.

Lengo kuu la mbio za NBC Dodoma Marathon ni kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kuchangia kutoa ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wanaosomea taaluma ya ukunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Fedha wa Benki hiyo Waziri Barnabas alisema; “Kupitia mbio hizi za NBC Dodoma Marathon, tunalenga kuchangia katika kuboresha afya ya uzazi kupitia sapoti kwenye mapambano dhidi ya kansa ya shingo ya kizazi kwa wanawake na pia kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa taaluma ya ukunga nchini. Tunaamini kuwa kupitia shindano hili tuweza kuisaidia jamii yetu kupambana na changamoto hizi.”

“Kupitia ufadhili wa wanafunzi wa elimu ya ukunga itasaidia kukabiliana na upungufu wa wataalamu hao na hivyo kupunguza vifo vya kina mama wakati wa uzazi. Vilevile tunaendelea na msaada wetu katika mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi ambapo mpaka sasa tumeshakusanya zaidi ya shilingi milioni 500 zilizosaidia kufikia upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake zaidi ya 23,500 na matibabu kwa zaidi ya wanawake 1,300. Tunajivunia mafanikio haya” alisema.

Akizungumza kuhusu mchango wa Benki ya NBC kwenye sekta ya michezo nchini, Ndugu Barnabas alisema; ”Benki ya NBC inatambua na kuthamini sana umuhimu wa michezo katika ujenzi wa taifa hususan katika kutoa ajira na kuongeza pato la taifa. Hivyo basi, tumeendelea kuwekeza katika michezo ikiwemo udhamini wetu mkubwa wa ligi kuu ya soka Tanzania yaani NBC Premier League ambayo imekuwa na matokeo chanya sana kwa taifa letu. Tunajivunia kuwa wadau wakubwa wa michezo nchini”.

Waziri pia alitumia fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru taasisi ya ORCI ( Ocean Road Cancer Institute) na Benjamin William Mkapa kuwa wabunifu na kwa huduma wanazotoa ili kusaidia jamii kuimarisha afya ya mama na mtoto.

Vile vile aliwashukuru wadau wa mashirika na makampuni mbali mbali kama Sanlam, Jubilee General Insurance, Garda World, Cheknocrafts, Icea Lions Insurance, Metropolitan Life Insurance, Strategies Insurance, Hans Paul, SBC- Pepsi, na Aramex kwa udhamini wao ili kufanikisha mbio hizi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Julius Mwaiselage alisema kuwa taasisi hiyo inafurahia kujumuika tena katika mbio hizi jijini Dodoma baada ya mafanikio awali. “Dhamira yetu ni kuendelea kutoa elimu zaidi ya saratani ya shingo ya kizazi ili kuimarisha afya ya mama na mtoto nchini. Saratani ya Shingo ya Kizazi, ndiyo inayoongoza kwa kusababisha vifo vingi zaidi vinavyohusiana na saratani kwa wanawake nchini Tanzania. Jambo la kutia moyo ni kwamba saratani hii inaweza kuzuilika na kutibiwa iwapo itagundulika mapema. Na kwa kuimarisha afya ya mama na mtoto tunajenga taifa lenye uwezo zaidi. Ni jukumu letu kwa pamoja kuunga mkono serikali yetu katika kuongeza uelewa na kuchangia uimarishaji wa afya za mama na watoto kulinda kizazi kijacho.” Alisema.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa programu kutoka Benjamin Mkapa Foundation alisema. “Nina furaha kujumuika na NBC katika mbio hizi kwani fedha zitakazo patikana katika mbio hizi zitasaidia kusomesha wakunga zaidi na kuboresha huduma ya afya kwa mama na mtoto na hivyo kujenga taifa lenye afya bora, Tatizo hili ni kubwa na uhaba wa wataalamu hawa ni mkubwa hivyo tunawasihi watanzania kujumuika katika mbio hizi kuchangia upatikanaji wa fedha ili tuweze kukabiliana na uhaba huu kwa pamoja” alisema.

Usajili wa mbio za NBC Dodoma Marathon umefunguliwa rasmi hivyo washiriki wanaweza kujisajili kupitia tovuti ya www.nbc.co.tz na kuchangia kiasi cha TZS 30,000 kwa usajili au 25,000 kwa kundi la watu ishirini na zaidi. Kwa maelezo zaidi tembelea matawi na vituo vya usajili vitakavyowekwa na NBC.

Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC Waziri Barnabas, akiongea wakati wa uzinduzi wa mbio za NBC Dodoma Marathon ambazo zitafanyika Dodma Julai 23 mwaka huu. Mbio hizo zinafanyika kwa mara ya nne mwaka huu zikilenga kukusanya fedha kwa ajili ya kupambana na saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea ukunga
Viongozi na wadhamini mbali mbali wa mbio za NBC Dodoma Marathon 2023 wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa mbio hizo unaotarajia kufanyika Dodoma Julai 23. Mbio hizo zinafanyika kwa mara ya nne mwaka huu zikilenga kukusanya fedha kwa ajili ya kupambana na saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea ukunga.
Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi wa mbio za NBC Dodoma Marathon 2023 ambazo zitafanyika Dodoma Julai 23 mwaka huu wakifuatilia kwa makini uzinduzi huo. Mbio hizo zinafanyika kwa mara ya nne mwaka huu zikilenga kukusanya fedha kwa ajili ya kupambana na saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea ukunga.
Viongozi na wadhamini mbali mbali wa mbio za NBC Dodoma Marathon 2023 wakionyesha alama ya uendo wakati wa uzinduzi wa mbio hizo unaotarajia kufanyika Dodoma Julai 23. Mbio hizo zinafanyika kwa mara ya nne mwaka huu zikilenga kukusanya fedha kwa ajili ya kupambana na saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea ukunga.