November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kujenga kituo maalum cha magonjwa ya mlipuko

Na Mwandishi wetu

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga hekali 90 kwaajili ya ujenzi wa kituo maalumu cha magonjwa ya mlipuko (isolation center) ikiwemo ugonjwa wa Marburg katika Mkoa wa Kagera kutokana na mwingiliano na wananchi kutoka nchi jirani na Mkoa huo.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Mei 22, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge Bernabetha Kasabago Mushashu katika Mkutano wa kumi na moja kikao cha 30, Bungeni Jijini Dodoma.

“Tumeshapata heka 90 ndani ya Mkoa wa Kagera kwaajili ya kujenga Isolation center itayosaidia katika matibabu ya magonjwa ya mlipuko yatayoweza kujitokeza nchini.” Amesema Dkt. Mollel.

Amesema, Sambamba na kujenga kituo hicho kitacho kitachosaidia kuwatenga wagonjwa wenye magonjwa ya mlipuko, Serikali itaendelea kuboresha huduma katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa kutenga zaidi ya Bilioni 4 ili wananchi wa mkoa huo na nchi jirani waendelee kunufaika na huduma hizo.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, Kwa mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imekamilisha hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura (EMD) ambalo limegharimu shilingi milioni 560,000,000, jengo la uangalizi maalum (ICU) shilingi milioni 650,000,000, jengo la huduma za Mionzi (Radiology) shilingi milioni  237,000,000, nyumba ya mtumishi shilingi milioni 90,000,000.

Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amesema, pamoja na kuboresha miundombinu katika hospitali hiyo Wizara imefanya ununuzi na ufungaji wa mashine ya CT Scan ambayo imegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1,810,000,000 na tayari huduma zimeanza kutolewa katika hospitali hiyo.