November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaombwa kuwaangalia wagonjwa wa Lupus

Na Penina Malundo, timesmajira

MKURUGENZI na Mwanzilishi wa Taasisi ya Lupus Tanzania(LUPUSTZ) ,Madam Irene Kilumanga ameiomba Serikali kuendelea kuwaangalia kwa ukaribu wagonjwa wa ugonjwa wa Lupus nchini hususan katika masuala ya matibabu ambapo dawa zao zimekuwa za gharama kubwa.

Pia ameiomba serikali kuangalia namna ya kufungua klinki ya kupima damu nchini ili kuweza kupunguza gharama za kupeleka damu nje ya nchi ambayo inachukua muda mrefu kwao katika kupata majibu na kupelekea wagonjwa wengine kufariki dunia kabla ya kupata majibu yao.

Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa Lupus nchini inayoendana na utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya uelewa wa ugonjwa huo,Kilumanga alisema licha ya serikali kwa sasa inaendelea kutoa uelewa juu ya ugonjwa huo lakini dawa za ugonjwa huo zimekuwa zinapatikana kwa gharama kubwa na zinapatikana katika maduka ya dawa makubwa.

Amesema Lupus haina tiba hivyo dawa wanazotumia ni za kupunguza ukali wa ugonjwa lakini sio kutibu ugonjwa huo.”Serikali inajitahidi sana kwa sasa katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa Lupus ambapo kwa sasa hadi wataalam nao wameweza kuongezeka katika hospitali mbalimbali ikiwemo hospitali ya taifa Muhimbili lakini kwenye suala la dawa hasa kwa watu ambao hawana bima za afya wanapata changamoto kubwa kupata dawa hizo lakini pia hata hao wenye bima za afya kuna dawa ambazo hawazipati katika bima hizo,”amesema na kuongeza

”Kwa hali hii watu wenye kipato cha chini kuweza kugharamia matibabu haya ni ngumu kwani dawa zimekuwa za gharama kubwa,”amesisitiza.

Amesema taasisi yake imekuwa ikiungana na wagonjwa wengine ambao wanaumwa ugonjwa huo na kuweza kuwasaidia baadhi ya wengine ambao wanapata changamoto mbalimbali za kupata matibabu kwa kuwawezesha dawa.

Kilumanga amesema kutokana na ugonjwa huu kutokuwa na takwimu maalum za wanaougua zinafanya serikali kushindwa kutupia macho hivyo ni vema wataalam wa utafiti sasa waanze kufanya utafiti kwa vitendo kwa ugonjwa huu ili kupata data kamili kwa wagonjwa wanaoumwa.

Kwa Upande wake Mwanzilishi wa Taasisi ya Lupus Awareness and Support (LASF),Hajjrath Mohammed amesema kwa sasa anamiaka 17 anaishi na ugonjwa huo ambapo amekuwa anapata changamoto kubwa katika upataji wa dawa kwani ununua nusu dozi ya dawa moja kwa kiasi cha sh. 700,000 ambapo hali yake ya kifedha haipo vizuri.

”Tunapotumia hizi dawa tunatumia kwa lengo la kupunguza makali ya ugonjwa huu,yaani yale mashambulizi yasiwe makubwa ila sio tunatumia dawa kwaajili ya kupona,na asilimia 90 ya waathirika wakubwa wa ugonjwa huu ni wanawake kuliko wanaume,”amesema.

Amesema kwa sasa hali yake imekuwa inazidi kudhorota ambapo makali yameanza kumshambulia na kumsababishia vidonda katika mdomo wake na ngozi imezidi kukakama na kumfanya kupata maumivu makali.