November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yashirikiana na Serikali katika uzalishaji

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MKURUGENZI Mtendaji Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Frank Nyabundege amesema,Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wenye tija hususan wa maziwa na samaki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma baada ya kuwasilishwa kwa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2023/24,Mkurugenzi huyo amesema,hatua hiyo itasaidia watanzania kujiajiri lakini pia kujipatia kipato cha kujikimu.

“Na sisi kama benki ya Maendeleo ya Kilimo tumekuwa tukishirikiana na Wizara hii kwa mfano kuna mradi tunauita TIDB ambao ni mradi wa kuhakikisha kwamba tunakuza uzalishaji na uchakataji wa maziwa nchini kwa sababu Tanzania ni kati ya nchi mabazo ukiangalia uzalishaji au unywaji wa maziwa upo chini,”amesema na kuongeza kuwa  

“Kwa hiyo kwa kushirikiana na wizara ambao nia yake ni kuhakikisha kwamba tunakuza uzalishaji kwa maana ya kwamba wafugaji wanaongeza tija katika kuzalisha maziwa nchini,kwa mfano kumekuwepo na wafugaji ambao wanafugaji kwa tija ndogo ,mfano mtu anaweza kupata lita tatu kwa siku au lita moja na nusu  wakati wenzetu wanafuga na kupata lita 30 na wengine hadi lita 60.”

Kwa mujibu wa Frank lengo la mradi huo ni kuhakikisha kwamba  wanawakwamua wafugaji  kutoka katika ufugaji wa kizamani ambao hauna tija na kwenda kwenye ufugaji wa kisasa kwa lengo la kuleta tija zaidi hasa katika uzalishaji wa maziwa.

“Lakini pia baada ya kupata maziwa mengi tutahitaji kuchakata na suala hilo limo ndani ya mradi huu..,tunapokuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao halafu hayachakatwi tunajikuta kwamba hatufikii lengo linalohitajika.”amesema

Mkurugenzi huyo amesema,hapa nchini kumekuwa na wafugaji wengi ambao wanafuga kizamani na hivyo kuwa na uzalishaji mdogo wa maziwa wa wastani hadi wa lita moja na nusu kwa siku hali ambayo amesema inachelewesha wahusika kupiga hatua za kimaendeleo.

Vile vile amesema,kaktika kuendeleza jitihada mbalimbali zikiwemo za kukuza ajira pia amesema serikali imekuwa na mradi wa uvuvi ambapo Wizara imetoa jumla ya shilingi bilioni 32 ambazo zinakwenda kutengeneza vizimba na kununua boti ambazo zitakwenda kufanya uvuvi katika bahari katika maziwa yaliyopo nchini kwa ajili ya kukuza uchumi wa Buluu suala ambalo amesema wanashirikiana na Wizara hiyo.

“Na katika bajeti ya Wizara kuna mambo mengi ambayo yanakwenda kufanyika, na sisi kama Benki ya Kilimo Tutashirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kwamba tunaendelea kukopesha sekta ya mifugo na uvuvi ili watanzania wakaneemeke na jinsi ambavyo benki ya TADB imekuwa ikitoa mikopo katika sekta hizo”

Ametumia nafasi hiyo  kuipongeza bajeti hiyo  nzuri kwa sababu imeonyesha ambavyo kumekuwa na ukuaji katika sekta hizo lakini pia malengo ambayo serikali ilitaka kuyapeleka mbele.

Aidha ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu kwa kuipa benki hiyo mtaji mkubwa kwa ajili a kuwakopesha wnawake na vijana ambao watafanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.