November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanarukwa watakiwa kuchangamkia fursa ujenzi wa ndege

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Sumbawanga

WAZIRI wa ujenzi na uchukuzi, Makame Mbarawa amewataka wakazi wa mkoa wa Rukwa kujipanga katika kuchangamkia fursa mpya kutokana na serikali kujenga uwanja wa ndege wa kisasa katika mji wa Sumbawanga Mkoani humo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa ujenzi wa uwanja huo baina ya Wizara ya ujenzi na uchukuzi na kampuni ya Beijing Construction Engineering Group Company Ltd ambayo itatekeleza mradi huo alisema kuwa hii ni fursa mpya kwa wakazi wa mkoa huo ambayo itawanufaisha.

” Baada ya kukamilika ujenzi na kuanza kutumika kwa uwanja huo, sekta ya Utalii Mkoani Rukwa itakua zaidi, uwekezaji utaongezeka, biashara katika mazao ya kilimo na uvuvi itaongezeka sambamba na biashara ya usafiri na usafirishaji itakua hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuona fursa iko wapi” alisema Waziri Mbarawa.

Aidha waziri huyo aliwaonya wakazi wa mkoa huo kutohujumu mradi huo pamoja na mingine kwa kuiba vifaa vya ujenzi, mafuta ya mitambo na saruji kwani kwa kufanya hivyo ni kuihujumu serikali kwakua ujenzi huo utagharamiwa kwa fedha za mkopo wenye masharti nafuu kutoka benki ya biashara ya Ulaya hivyo kufanya hivyo ni kujiibia wenyewe.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji mkuu wa Tanroads Mhandisi Rogatus Mativila alisema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa thamani ya Tsh. bilioni 55.9 ambapo utahusisha ujenzi wa eneo la kutua ndege, eneo la maegesho ya ndege, jengo la ofisi ya kuongozea ndege pamoja na jengo la wageni.

Alisema kuwa pia utafanyika ujenzi wa barabara ya kuingia na kutoka uwanjani hapo, maegesho ya magari, uzio kuzunguka uwanja, kufunga taa maalumu zitakazo ruhusu safari za ndege kufanyika usiku na mchana katika kipindi chote cha mwaka.

Mtendaji huyo alisema utekelezaji wa mradi huo utachukua miezi 18 pia muda wa matazamio wa mradi utakua miezi 12 ambapo aliahidi kuwa Tanroads watahakikisha wanamsimamia mkandarasi huyo ili atekeleze mkataba kwa ubora na kwa wakati kadiri mkataba ulivyo sainiwa.

Akitoa taarifa ya mkoa, Mkuu wa mkoa wa Rukwa Queen Sendiga alisema kuwa wananchi wamekuwa wakiusubiri mradi huo kwa muda mrefu na wako tayari kusafiri kwa ndege kwani uchumi wa mkoa wa Rukwa unaruhusu kwakua wananchi wake ni wakulima na wanafedha.

Alisema serikali ya mkoa wa Rukwa itampa ushirikiano wote mkandarasi ikiwemo ulinzi wa vitendea kazi eneo la mradi ili mradi huo ukamilike kwa wakati kwa kua mkoa wa Rukwa hautaki miradi inayosuasua kwani wananchi wanataka maendeleo ya haraka na ukikamilika kwa wakati itakua ni fursa nzuri ya kupata mradi mwingine.

Kwaupande wake Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga mjini, Aesh Hillary alimshukuru Rais Dkt. Samia Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa uwanja huo kwani kwa miaka mingi wananchi wa Sumbawanga walikua wakiungojea uwanja huo ambao utakwenda kufungua fursa nyingi za kiuchumi Mkoani humo.

Mkuu wa mkoa Rukwa Queen Sendiga akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini ujenzi wa uwanja wa ndege mkoani Rukwa