November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndalichako:Serikali inatambua umuhimu wa nguvukazi ya Taifa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Ajira na Wenye ulemavu,Prof.Joyce Ndalichako amesema serikali inatambua umuhimu wa kulinda nguvukazi ya Taifa  hivyo inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 lengo ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kazi Nchini yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Amesema kuwa amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameboresha  usalama wa watumishi mahali pa kazi .

Ndalichako amesema hayo jijini hapa leo Aprili 26,2023 wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi Duniani  itakayoadhimishwa Aprili  28 mwaka huu mkoani Morogoro.

Ametaja lengo kubwa la maadhimisho hayo kuwa ni  kuendeleza kampeni za kuhamasisha na kuweka mazingira salama katika sehemu za kazi ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Mazingira Salama na Afya kazini ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi”.

Aidha ameeleza kuwa kutokana na takwimu za kidunia zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO)  mwaka 2022 zinaonesha kwamba zaidi ya watu milioni 2.9  hupoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Ambapo kati ya watu hao  zaidi ya wafanyakazi milioni 402 uumia wakiwa kazini na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi chote wanachopatiwa matibabu hadi hapo watakapopona.

Alifafanua kuwa kwa upande wa  Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249 ambapo katika ajali hizo, vifo vilikuwa 217.

“Takwimu hizo ni kubwa sana zinaathiri utendaji kwa kuwa zinasababisha upotevu wa maisha ya Wafanyakazi na pia kuathiri shughuli wakati wafanyakazi walioumia wakiendelea kupata matibabu. Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kwamba suala la ajali na  magonjwa yatokanayo na kazi linahitaji jitihada za makusudi katika kukabiliana nalo,”amesema.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA Khadija Mwenda amesema kuwa  katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa Kazi tarehe serikali kwa kushirikiana na wadau itaendesha kampeni maalum ya uhamasishaji .

Amesema uhamasishaji huo utakuwa kwa njia ya mafunzo ya Usalama na Afya miongoni mwa makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo pamoja na watu wenye ulemavu.