November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. (Picha na Mtandao).

Uteuzi wa Gambo, Daqarro, Dkt. Madeni watenguliwa

Na Mwandishi Maalum, TimesMajira Online

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli Juni 19, mwaka huu ametengua uteuzi wa viongozi watatu wa Mkoa wa Arusha na kufanya uteuzi wa viongozi watakaoshika nyadhifa zao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa imebainisha kuwa, kwanza Rais ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na amemteu, Idd Kimanta kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Kabla ya uteuzi huo, Kimanta alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli mkoani Arusha na nafasi ya mkuu wa wilaya hiyo itajazwa baadaye.

Pili, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro na amemteua Kenan Kihongosi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Kabla ya uteuzi huo, Kilhongosi alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa.

Aidha, jambo la tatu Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt.Maulid Madeni na amemteua, Dkt,John Pima kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Kabla ya uteuzi huo, Dkt.Pima alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.

Pia, Rais Dkt.Magufuli amemteua, Jerry Mwaga kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua ambaye kabala alikuwa Afisa katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Kwa mujibu wa Msigwa, wateule wanatakiwa kuwepo Ikulu jijini Dar es Salaam Juni 22, mwaka huu saa 2:30 asubuhi.