November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mwinyi mgeni rasmi maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari

Na Mwandishi wetu, timesmajira

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussen Mwinyi anatarajia kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari nchini,Mei 3 mwaka huu ambapo maadhimisho hayo yataambatana na mijadala mbalimbali ikiwemo masuala mabadiliko ya sheria ya vyombo vya habari.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari,Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania, Dkt. Rose Reuben amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo yanayotarajia kufanyika kitaifa Zanzibar yanalenga kukuza uelewa wa umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na kukumbusha Serikali na jamii umuhimu wa kuheshimu na kulinda haki ya uhuru wa habari.

Amesema maadhimisho ya mwaka huu ni ya 30 kuadhimishwa yanaangazia uhuru wa vyombo vya habari,pamoja na vyombo huru vya habari kama ufunguo muhi mu wa kufurahia haki nyingine zote za binadamu.

”Mwaka huu,TAMWA ni mwenyekiti wa kamati ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani hapa nchini,hivyo inapendekeza kwa wadau wa habari na serikali kutoa kipaumbele kwa haki ya uhuru wa kujieleza,uhuru wa vyombo vya habari,usalama wa wanahabari na uhuru wa kujieleza kwani unazidi kushambuliwa jambo ambalo linaathiri utekelezaji wa haki nyingine za binadamu,”amesema na kuongeza.

”Uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi ya binadamu ambayo ni muhimu kwa jamii ili kuwa ya kidemokrasia na inawezesha kubadilisha uhuru wa mawazo,maoni na taarifa na hivyo kuruhusu wanajamii kutoa maoni yao kuhusu masuala yenye tija kwa umma,”amesema Dkt. Reuben.

Amesema vyombo vya habari vinaweza kuwa huru na kutimiza jukumu lake la kuhabarisha umma juu ya mambo kadha wa kadha kama kutakuwa na uhuru wa kujieleza katika jamii na sekta huru ya vombo vya habari .”Sekta hii ya habari ni huru na ni sekta ambayo inaweza kuwafahamisha jamii na kuwawajibisha viongozi,”amesema Dkt. Reuben.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo,Rodney Tadeusi amesema serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wa habari ambapo mwaka jana maadhimisho hayo yalibahatika kuhudhuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,hii ni namna ambavyo serikali inaenzi siku hiyo.

‘Kama ilivyoada Serikali italinda uhuru na kuunga mkono maazimio yanayotolewa na wadau yanayolenga kuhakikisha sekta ya habari inaendelea kuimarika na uhuru wa habari unaendelea kupanuka zaidi na wananchi kuwa na uhuru wa kujieleza,”amesema na kuongeza

”Serikali inaenda kuadhimisha siku hii huku ikiwa imefanya mambo mbalimbali ikiwemo kubadilisha sheria mbalimbali ambavyo kwa njia moja au nyingine zilikuwa zinaonekana kama zinaweka uzito katika sekta ya habari,”amesisitiza.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Umoja wa Mataifa nchini,Nancy Angulo amesema kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya siku hiyo inaendana na azimio la haki za binadamu.”Katika kusherekea kutimiza agenda ya malengo endelevu y mwaka 2030 ,madhimisho hayo yanatoa nafasi ya kuhimiza uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza kama haki ya binadamu,”amesema.