Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Walimu wa sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Wilayani Ilala wamepatiwa mafunzo kuhusu mtaala mpya wa ujenzi wa umahiri (Competence Based Curriculum) ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika masomo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Zanaki, Mkuza Mitaala kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Sophia Amasi, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha walimu kutekeleza mtaala huo kwa mafanikio.
“Mtaala umeandaliwa kujenga umahiri kwa mtoto utakaomwezesha kumudu ujifunzaji, huu ni mfumo mpya wa ufundishaji ambao unaendelea kutumika, tunatarajia baada ya mafunzo walimu watakuwa wamepata mbinu bora tutaongeza ufaulu wa wanafunzi,” alisema Amasi.
Alisema walimu wanafundishwa mbinu za ufundishaji na ujifunzaji na namna ya kutunga maswali ya ujenzi wa umahiri na kufanya tathmini inayozingatia ujenzi wa umahiri.
Alisema wanatarajia kuwafikia walimu wote Tanzania na tayari wametoa mafunzo hayo katika Wilaya za Mbarali, Kibiti na Kisarawe.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Zanaki, Delvine Koka, aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuwaandalia mafunzo hayo na wawezeshaji TET kwani yatawawezesha kuufahamu mtaala huo vizuri.
“Mtaala wa ujenzi wa umahiri ni mpya walimu wengi bado hawana ufahamu kwa hiyo mafunzo kama haya ni muhimu,” alisema Koka.
Mmoja wa walimu walioshiriki, Kudra Hashimu wa Shule ya Sekondari Mnazi Mmoja, alisema watatumia mafunzo hayo kwa ufasaha ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi. “Mfumo wa awali wanafunzi wengi walikuwa wakikariri lakini huu wa sasa wa ujenzi wa umahiri utapima vizuri uelewa wa mwanafunzi,” alisema.
Mwalimu mwingine Nchwembu Fabian wa Shule ya Sekondari Zanaki, alisema mafunzo yatawawezesha kufahamu mbinu bora za ufundishaji na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa