November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Same aazisha tuzo kwa shule zitakazofanya vizuri na zawadi ya kinyago kwa zitakazo fanya vibaya

Na Martha Fatael, Timesmajira Online,Same

MKUU wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni ameanzisha tuzo maalumu ya serikal kwa ajili ya kuzitoa kwa Shule zitakazofanya vyema katika mitihani ya taifa kuanzia Julai mwaka huu.

Aidha serikali wilayani hapa imeahidi kutoa Kinyago kwa shule zitakazofanya vibaya katika mitihani hiyo huku Kinyago hicho kikipokewa na Diwani na Mkuu wa Shule husika.

Mgeni amesema hayo wakati wa kikao cha wadau wa elimu wa Wilaya hiyo kilicholenga kutafakari sababu za wilaya kufanya vibaya kati ya wilaya sita za Mkoa huo.

Amesema pamoja na kwamba wilaya inaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji, motisha kwa walimu, mazingira mazuri kwa wanafunzi kusoma, Mkuu wa Mkoa atakuwa Mgeni rasmi katika tuzo hizo.

Mkuu wa wilaya ametaja sababu nyingine za kushuka kwa Kiwango cha elimu ni watoto kufanyishwa biashara sokoni ili kulea familia.

Aidha baadhi ya shule za msingi zilizopo ukanda wa milimani mwa wilaya hiyo kuwa na wastani wa mwalimu mmoja hadi watatu huku ukanda wa tambarare ukiwa na walimu kati ya 16 na 18.Alitaja sababu nyingine kuwa ni wanafunzi kukosa chakula shuleni, wanafunzi kutembea umbali mrefu kufika shule na upungufu wa walimu.

Amesema sababu nyingine ni mmomonyoko wa maadili huku watoto wakibakwa na kulawitiwa na ndugu wa karibu wa familia.

Mapema Mkuu wa Divisheni ya Elimu Awali na Msingi wilayani Same, Marclaud Mero amesema wilaya hiyo ina jumla ya shule za msingi 203, zikiwamo 187 za serikali na 16 za taasisi binafsi.Huku kwa upande wa shule ya sekondari, wilaya ina shule 63, zikiwamo 43 za Serikali na 20 za taasisi binafsi na chuo kimoja cha ualimu ambacho ni binafsi.