Na Esther Macha,Timesmajira, Online,Mbeya
SPIKA wa Bunge,Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt.Tulia Ackson ametoa msaada wa mifuko 100 ya saruji ,bati bando mbili pamoja na na kiasi cha milioni 1 katika shule ya sekondari Kalobe kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika shule hiyo.
Dkt. Tulia amekabidhi msaada huo leo wakati alipofanya ziara katika shule ya Sekondari Kalobe iliyopo mkoani Mbeya baada ya kujionea uharibifu wa choo uliotokea katika shule hiyo.
Ambapo uharibifu huo ulitokea baada ya choo hicho kudondokewa na miti kutokana na mvua kubwa iliyonyesha wiki iliyopita.
Aidha amesema msaada huo utasaidia ujenzi wa vyoo hivyo katika kuwaongezea nguvu Halmashauri ya Jiji la Mbeya ili vyoo hivyo viweze kukamilika mapema.
Mmoja wa wazazi wa watoto katika shule hiyo, Jane Mwansele amesema kuwa walipata mshtuko baada ya vyoo hivyo kudondoka na kuamua kuitisha kikao na kuanza kuchimba mashimo.
Mwansele amesema ameeleza kuwa sababu ya vyoo hivyo kuanguka ni kutokana na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa hali ambayo imechangia wanafunzi kuathirika kimasomo kwani awali walikuwa wakirudi saa 11 jioni lakini hivi sasa wanarudi saa 8 mchana.
Hata hivyo Dkt Tulia pia ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Dkt. Tulia Ackson iliyopo katika Kata ya Itende.
Ambapo aliwataka wahusika kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ili kuwawezesha wanafunzi kupata huduma bora ya elimu ikiwemo miundo mbinu rafiki.
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Kalobe Songa Langson, amesema kuwa shule hiyo ilipata janga la kubomoka kwa choo iliyosabishwa na mvua kubwa.
Amesema kuwa shule imechukua hatua kwa kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya ambapo choo hicho kilikuwa na matundu 12,kutokana na changamoto hiyo walilazimika kufanya jitihada kwa wanafunzi wasichana watumie vyoo vya walimu vyenye matundu mawili wakati jitihada za kujenga choo kingine kinajengwa.
Aidha Mwalimu huyo amesema kuwa wanafunzi 453 kutumia matundu mawili ya choo si sawa kwa afya , na kusema kuwa kufuatia changamoto hiyo uongozi wa shule umeita wazazi ili kuona namna bora ya kutatua changamoto hiyo na wamekubaliana kuwa wazazi watachimba mashimo.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili