November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge, yaipongeza serikali kwa uwekezaji miradi ya umeme Kigoma

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Kigoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imeipongeza serikali kwa jitihada na  utekelezaji  wa miradi ya kupeleka  umeme wa gridi ya taifa mkoani Kigoma, miradi inayotekelezwa kupitia Shirika la Umeme nchini TANESCO.

Pongezi hizo zimetolewa  na Mwenyekiti wa kamati hiyo  Jerry Slaa kwa niaba ya kamati, wakati wa ziara  ya kukagua mashine za uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta katika kituo cha cha Bangwe mkoani Kigoma Machi 20, 2023  mashine zitakazozalisha jumla ya megawati 8.75.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya uwekezaji wa Mitaji ya umma, (PIC) Mhe. Jerry Slaa (katikati) akizungumzia juu ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya Umeme wakati Kamati ya PIC ilipokitembelea kituo cha kuzalisha na kusambaza umeme wa kilovoti 33/11 cha Bangwe, kilichopo Kigoma mjini, siku ya Jumatatu, tarehe 20 Machi, 2023.

Slaa, amesema kuwa serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha watanzania wanapata umeme wa uhakika  kwa kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya kuzalisha umeme na hasa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme  inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa njia ya umeme mkubwa wa kilovolt 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma,mradi ambao ukikamilika serikali itaweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika katika kuzalisha umeme kwa njia ya mafuta.

“uzalishaji wa umeme kwa mafuta ni dola senti 25 kwa unit,wa maji dola senti 5, umeme wa jua dola senti 4 na wa gesi ni dola senti 7  kwa unit moja  tunaona kabisa uzalishaji wa mafuta unavyougharimu serikali” alisema Slaa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji  wa TANESCO, Maharage Chande amesema  kuwa  mradi wa  ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovolti 400 kutoka  Nyakanazi  hadi Kigoma umekamilika kwa asilimia 47  na Kusema kuwa kazi ya kukamilisha mradi huo inaenda kwa kasi ili kuhakikisha mkoa wa Kigoma na maeneo ya jirani yanapata Umeme wa kutosha .

“mradi huu utakapokamilika tutazalisha umeme wa kutosha kuwasha Kigoma na kuweza kufanya biashara ya kuuza umeme nchi za jirani” aliongeza  Chande