November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uswis, Hispania na Unesco
kuimarisha utamaduni nchini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi kutoka Ubalozi wa Uswisi na Hispania nchini Tanzania na Wataalam wa masuala ya Utamaduni kutoka Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kujadili uendelezaji wa Sekta ya Utamaduni hapa nchini.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam leo, Yakubu ameushukuru ujumbe wa Mabalozi hao kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha Sekta ya Utamaduni hapa nchini hususani kwenye maeneo ya taarifa, uendelezaji ubunifu na kukuza lugha ya Kiswahili.

Amesema Wizara imetoa kipaumbele kwenye Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutokana na umuhimu wake katika kutoa ajira na kuchangia Pato la Taifa.

Ameongeza kuwa, mwaka 2022 Serikali ilianzisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi Wasanii kwa masharti nafuu ambapo umefanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.077 kwa waombaji 45 waliokidhi vigezo.

Aidha, ameueleza ujumbe huo kuwa Tanzania imefanikiwa kujiunga tena uanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Mabaraza ya Sanaa na Mashirika ya Utamaduni kutokana na kuimarika kwa sifa za Tanzania katika medani ya Diplomasia na Ushirikiano wa Kimataifa katika Sekta ya Sanaa kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wao wawakilishi wa Mabalozi hao wakizungumza wakati wa mkutano huo wameeleza kuwa wataendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza Utamaduni.

Wamesema, UNESCO imetenga siku maalum ya kuadhimisha Lugha ya Kiswahili duniani na kuongeza kuwa wataendelea kuweka nguvu katika kuangalia Diplomasia ya Utamaduni hususani kuongeza nguvu katika eneo la ubunifu, ushirikiano na kubadilishana uzoefu ili wananchi wengi zaidi wanufaike