November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aweso:wizara imekubali maombi ya MUWSA juu ya ujenzi wa bwawa la maji la Weruweru

Na Martha Fatael, TimesMajira online,Moshi

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso,’amenusa’ harufu ya ufisadi unaofanywa na baadhi ya Mamlaka za Maji nchini kwa kisingizio cha upotevu wa maji baada ya kuzalishwa.

Aidha waziri Aweso amesema wapo baadhi ya watumishi wasio waaminifu ambao uuza maji hayo kwa taasisi ama hoteli kubwa kisha fedha hizo huingia mifukoni mwa watu wachache.

Aweso amesema hayo wakati anazindua Bodi mpya ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) na kutaka bodi hiyo kuandaa mipango ya kupunguza kiwango Cha maji yanayopotea.

Ametoa mfano wa moja ya mamlaka nchini hapa bila kuitaja jina kwamba ina upotevu wa maji kwa asilimia 40 jambo ambalo linatia mashaka na kuhitaji ufuatiliaji wa karibu kuona hicho kiwango kinachopotea kiko wapi.

Kuhusu taarifa ya MUWSA kuwa na upotevu wa maji wa asilimia 27.35,ameagiza mipango iandaliwe na upotevu huo ushuke hadi chini ya asilimia 20 ili wananchi wapate maji ya uhakika.

Aweso amesema wizara imekubali maombi ya MUWSA juu ya ujenzi wa bwawa la maji la Weruweru na inatafuta wafadhili kwa ajili ya bwawa hilo litakaloongeza huduma ya maji maeneo ya Moshi, Mji Mdogo wa Bomang’ombe na Hai.

Kuhusu upanuzi wa mabwawa ya maji taka Wizara inatambua umuhimu wa mfumo huo na imetenga fedha kwa ajili ya kuunganisha Kiwanda cha Ngozi.Aidha waziri ametaka mamlaka kutoza ankara halali za maji kwa wateja wao na badala yake walipe kulingana na matumizi yao.

Awali Mkurugenzi wa MUWSA, Mhandisi Kija Limbe amesema mamlaka hiyo inaendelea kuboresha huduma katika maeneo yote ya manispaa pamoja na wilaya za pembezoni.