November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NDC na TEMDO wameingia makubaliana ya kimkakati ya kupunguza gharama viwandani

Na David John, Timesmajira Online

MKURUGENZI wa Shirika la maendeleo la Taifa (NDC) Dkt Niclous Shombe Amesema limeingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika bobezi la utafiti, uchoraji na utengenezaji mitambo la TEMDO ambapo ushirikiano huo umetajwa utasaidia kupunguza gharama za uagizaji mitambo na vipuri kwenye viwanda vya hapa nchini.

Hayo ameyasema Machi 16 2023 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za Shirika la Maendeleo la Taifa NDC ambapo DKt amesema ushirikiano huo utafanyika kupitia kiwanda cha kuzalisha mitambo cha Kilimanjaro (KMT) ambapo wataalamu wa TEMDO watabuni, na watachora pamoja na kutengeneza mitambo kwa ajili ya viwanda vya ndani na nje ya nchi.

“Kiwanda cha KMT kinamilikiwa na NDC, sasa ushirikiano huu na TEMDO utawezesha wataalam wetu kushirikiana na wale wa TEMDO kuzalisha mitambo ambayo itatumika kwenye viwanda vyetu, hivi viwanda vya humu ndani vinatumia gharama kubwa kuagiza vipuri au mitambo kamili nje ya nchi, sasa kwa ushirikiano huu tutaweza kupokea oda ya mtambo unaotakiwa na wataalam wetu wakaufanyia usanifu na kutengeneza hapa hapa kupitia kiwanda cha KMT,” amesema Dk Shombe.

Nakuongeza kuwa “TEMDO ni wabobezi kwenye utafiti na uzalishaji wa mitambo hivyo watakuwa kituo chao cha utafiti wa mitambo nakwamba milango Iko wazi kushirikiana na sekta binafsi.”Amesema Dkt Shombe

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO, Profesa Frederick Kaimba, amesema ushirikiano walioingia na NDC utawafanya kufanya utafiti na kwenda kuzalisha KMT mitambo na vipuri mbalimbali.

Amesema kuwa Kwa kupitia ushirikiano huo wanaweza kusanifu na kuzalisha minara inayoweza kutumika kusafirishia umeme kwenye mradi wa bwawa la umeme la mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).

” Uwezo huo tunao…,na pia tunaweza tukasanifu na kutengeneza Mashine za kuchakata miwa na kupata Sukari, kwa ujumla ushirikiano huu una manufaa makubwa kwa nchi, utapunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza vifaa nje ya nchi lakini pia unaweza kuleta ajira kwa watanzania,” amesema Profesa Kaimba.

Pia amesema ushirikiano huu unakuja kuziba nafasi ya wataalam walioondoka baada ya kipindi cha ubinafsishaji wa viwanda.

“Viwanda vyetu vimepitia hatua mbalimbali kama hatua ya ubinafsishaji, sasa ushirikiano huu unakuja kuziba mapengo yaliyokuwepo hasa kwenye uzalishaji, na mitambo na Mashine zitakazozalishwa zitakuwa matumizi ya viwanda vya hapa nchini lakini pia nje ya nchi pale tutakapopokea oda,” amesema Profesa Kaimba.

Profesa Amesema makampuni na viwanda binafsi vina nafasi ya kupunguza gharama zao za kuagiza vifaa nje ya nchi kama watatoa fursa kwa KMT kutengeneza vifaa wanavyovihitaji.