November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ZFDA walifungia ghala lililokuwa linahifadhi bidhaa mbalimbali kwa kukosa sifa

Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline,Zanzibar

Wakala wa chakula na dawa Zanzibar ZFDA wamelifungia ghala   iliyokua ikihifadhi bidhaa mbalimbali ikiwemo mchele  kutokana na ghala hiyo kukosa sifa za kuhifadhia bidhaa hizo.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa kushtukiza kuangalia usalama wa chakula,na uhalali wa uwepo wa ghala hilo huko Mpendae Kaimu Mkurugenzi Idara ya usalama wa chakula ZFDA  khadija Ali Sheha amesema   ukaguzi umebaini kuwa ghala hilo halijasajiliwa,haliko katika hali ya usafi na  haliruhusu hewa kupita hali inayopelekea chakula kinachihifadhiwa hapo kutokua salama.

Alisema kuwa usalama wa chakula ni jukumu la Kila mmoja  hivyo ameitaka jamii kutoa taarifa mapema mara tu wanapoona Hali isiyokuwa ya kawaida katika maghala ya kuhifadhia chakula

“Kwapamoja sasa tushirikiane kulinda Afya zetu  kwa kuyafichuwa maghala kama haya ambayo yanahatarisha Afya za watu na kuitia hasara Serikali” alishauri kaimu huyo.

Aidha katika ukaguzi huo ZFDA wamebaini Kua mmiliki wa ghala hilo amekua akiziba vifungashio vya asili Kwa baadhi ya  bidhaa zilozuiliwa kusafirishwa nje ya Zanzibar ikiwemo mchele aina ya mapembe  katika maboksi na vipolo ili kurahisisha usafirishaji   Jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kwa upande wake mmiliki wa ghala hilo Saleh Hassan Khamis amesema kuwa amekua akizifunga tena bidhaa hizo katika mapolo na maboksi ili kuzihifadhi na kuziweka salama wanapokua safarini bila kufahamu kufanya hivyo kama ni kosa kisheria, hivyo saleh ameiomba ZFDA kuwapatia  elimu Wafanyabiashara ili kuepuka makosa yasiyotarajiwa.

Nae Sheha wa Shehia ya Mpendae suleiman Ali Makuu amewasihi wafanya Biashara kuwa waaminifu na kuwataka  wafuate  Sheria zilizowekwa na Serikali ili kuepuka matatizo wakati wanapofanya Biashara zao.

Katika Ukaguzi huo  mbali na bidhaa nyengine jumla ya polo mia tatu za mchele aina ya mapembe yenye ujazo wa kilo hamsini yamekutikana  katika ghala hilo ambalo halijasajiliwa.