November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mawakala wa mabasi Tabora waonywa kuvamia abiria.

Na Allan Ntana, Tabora 

UMOJA wa Mawakala hao wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani mjini Tabora umewataka mawakala wake kuacha mara moja tabia ya kukimbilia na kung’ang’ania abiria wanaofika kwenye vituo vya mabasi mjini hapa kupata huduma ya usafiri badala yake wazingatie taratibu,kanuni na sharia walizojiwekea ili kuleta tija katika utendajikazi wao.

Wito huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa umoja huo Mkoani hapa Said Wankyo alitoa wito wakati akiongea na gazeti hili ambapo alisema kuwa tabia hiyo imekuwa ikiwapa usumbufu mkubwa sana abiria wanaokuja kutafuta usafiri katika kituo hasa nyakati za alfajiri na asubuhi.

Wankyo alisema kuwa mawakala hao wanapaswa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na umoja huo na kuacha abiria kuingia vituoni na kupata huduma wanazohitaji katika ofisi za mabasi husika na siyo kuwavamia.

Alisema kuwa mawakala wanatakiwa kuzingatia sheria zote walizojiwekea ikiwemo kuvaa sare safi,vitambulisho,kuanza kazi kuanzia saa 10:30 alfajiri hadi saa 4:30 usiku na kuwa na lugha nzuri kwa abiria na watu wengine wanaoingia katika vituo hivyo ili kuvutia na kuleta tija katika utendajikazi wao.

Aliwataka kuacha mara moja tabia hizo na vitendo vyote viovu ambavyo kisheria havikubaliki ikiwa ni pamoja na ulevi,matusi,kushiriki katika matukio ya wizi na kushirikiana na vibaka kuwaibia abiria ambapo wanatakiwa kuwa wazalendo na waaminifu zaidi katika utendajikazi kwa kujitolea kuwasaidia abiria kwa hali na mali pindi waingiapo kwenye vituo hivyo.

“Tumejiwekea taratibu,kanuni na  sheria zinazotuongoza ili kuondoa ubabaishaji lakini kuna baadhi ya wenzetu wanazivunja kwa makusudi wakidai wanatafuta maslahi kitu ambacho kinaharibu sifa na kushushia heshima wengine,tunaendelea kuelimishana na kuchukuliana hatua za kisheria pale mtu anapokiuka na kuvuka mipaka ya kazi”alisema.

Mwenyekiti huyo alitahadharisha abiria kuwa makini na mawakala ambao hawafuati sheria  kwa kuwavamia, kuwang’ang’ania na kuwanyang’anya mizigo yao ili kuwahudumia pindi wanapofika katika vituo hivyo kupata huduma mbalimbali ambapo amewataka kukataa,kutoa taarifa kwenye kituo cha Polisi kilichopo kituoni hapo au kwenye ofisi ya Meneja wa kituo hicho ili wapatiwe msaada zaidi.

Aidha aliwataadharisha watu wote ambao hawana shughuli maalum katika vituo hivyo kutoingia na kufanya uhalifu kwa kuwa hivi sasa Jeshi la Polisi linafanya doria kali mara kwa mara kuwabaini wahalifu wote wanaoibia abiria mali zao na kuhatarisha usalama wao pomoja na mali nyingine zilizopo kwenye maeneo hayo.

Wankyo alisema kuwa kuna kundi la watu wanaojulikana ambao hawana shughuli rasmi wanaojipenyeza na kuingia katika vituo hivyo kwa lengo la kufanya uhalifu ambapo majina yao yamepelekwa kwa Jeshi la Polisi ili kuwafuatilia na kuwakamata katika kupambana kudhibiti vitendo vyote viovu kwenye maeneo hayo.

Alisisitiza kuwa umoja huo utahakikisha hakuna abiria atakayeingia katika vituo hivyo anasumbuliwa na utasisimia amani na usalama wao pamoja na mali zao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kwamba hautakubali kuchafuliwa na watu wachache ata kama ni wanachama wao ama watu wanaojifanya kuwa mawakala ili kutekeleza vitendo vya uhalifu.