Na David John, Timesmajira Online DSM
JAMII imehamasishwa kuongeza nguvu katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuondokana na athari za mazingira huku matumizi ya nishati safi ya kupikia yakitajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuendeleza uchumi kuanzia ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa machi 15 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Shirikisho la Kampuni za Gesi nchini Tanzania, Araman Benoite ambaye pia ni Mkurugenzi wa Oryx Gas nchini alipokuwa akizungumza kwenye Kongamano la Kampuni za Gesi Afrika Mashariki linaloendelea jijini humo.
“Tutumie fursa ya gesi ya kuwekeza ili kuwafikia wananchi wengi ambao bado hawjaanza kutumia nishati safi ya kupikia. Pia tuitumie fursa hiyo kuwekeza na kuimarisha uchumi,” amesema Benoite.
Benoite ameongeza kwamba bado kuna fursa ya uwepo wa soko kubwa la gesi ya majumbani kwani Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipambanua kuhamasisha matumizi yake.
Akizungumzia umuhimu wa kufanyika kwa kongamano hilo amesema ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ina faidi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Benoite, miongoni mwa faida hizo ni pamoja na kusaidia mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira, kuunga mkono jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutumia muda mchache katika shughuli za mapishi tofauti na pale endapo wangetumia nishati nyingine kupikia kama Kuni au mkaa.
Akifafanua kwa nini kongamano hilo limefanyika Tanzania, amesema ni moja ya mkakati wa Kampuni za gesi kuunga mkono jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Samia kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati ya gesi.
Kongamano hilo limehudhuriwa na wadau kutoka nchi mbalimbali ikiwamo za Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na kampuni za Kimataifa zinazokijusisha na biashara ya gesi duniani.
Awali akisoma hotuba ya ufunguzi wa kongamano hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mkurugenzi wa Shirikisho hilo duniani Catherine Ho, alisema kongamano hilo litakuwa jukwaa muhimu katika kuongeza uelewa na kukuza uwekezaji katika sekta ya nishati hususan gesi ya majumbani (LPG) nchini Tanzania.
Ameongeza kuwa zaidi ya washiriki 800 walisajiliwa katika kongamano hilo wakiwemo wataalamu wa nishati ambapo pamoja na mambo mengine wataonyesha jinsi sekta hiyo ilivyo muhimu katika kukuza uchumi.
Pamoja na mambo mengine kwenye Kongamano hilo la Kimataifa,pia wameanzisha Shirikisho ngazi ya Tanzania ambalo litakuwa likisimamia na kutoa muongozo kuhusu masuala mbalimbali kwenye sekta ya nishati ya gesi.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti