October 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shekilindi awataka wananchi Makanya kumuunga mkono Samia

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Lushoto

MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu kama Bosnia, amewataka wananchi wa Kata ya Makanya kuendelea kumuunga mkono Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchangia nguvu zao kwa miradi inayopelekwa kwenye kata hiyo.

Ni baada ya Machi Mosi, 2023 kutembelea miradi iliyopo kwenye Kata ya Makanya, huku akiwa ameongozana na baadhi ya Wakuu wa Idara ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.

“Wananchi naomba muendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za miradi anazoleta kwenye kata ya Makanya. Fedha hizo ni nyingi, lakini zitafanya kazi nzuri zaidi kama na ninyi mtaweka nguvu zenu” alisema Shekilindi ambaye aliweza kutembelea miradi iliyotekelezwa kwa fedha kutoka Setikali Kuu, halmashauri na michango na nguvu za wananchi.

Miradi aliyotembelea Shekilindi, na kuongozwa na Ofisa Mtendaji Kata ya Makanya Emiliana Kajula, ni ile iliyopo Shule ya Msingi Mboghoi katika Kijiji cha Mdando, ambapo wananchi wamejenga vyumba vitatu vya madarasa na ofisi moja ya walimu hadi usawa wa linta, na hadi sasa sh. 10,543,000 zimetumika. Pia Serikali Kuu imetoa sh. milioni 6.6 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo, lakini ili kuweza kukamilisha ujenzi huo ni lazima wananchi wachimbe shimo, wasombe mawe, mchanga na kokoto.

Diwani wa Kata ya Makanya Zanuali Mohamed alisema kwa hatua hiyo ya wananchi kujenga vyumba vitatu vya madarasa na ofisi moja ya walimu, ipo haja ya Serikali kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo ili kuongeza vyumba vya madarasa kwa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1974, lakini hadi sasa ina vyumba vya madarasa vitano tu kuanzia darasa la kwanza hadi la saba. Hivyo, ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi 604, kunahitajika vyumba 14 vya madarasa.

Shekilindi pia alifika Shule ya Sekondari Mdando, ambapo kuna ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na ofisi mbili, ambapo shule hiyo ilipata sh. milioni 80 kutoka Serikali Kuu kupitia fedha za tozo, na ujenzi umekamilika.

Mradi wa Shule ya Msingi Bosha, Kijiji cha Bwaya, kulikuwa na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, ambapo wananchi walianza mpaka linta, na Umaliziaji wa darasa moja lilimaliziwa kwa fedha za EP4R, na jingine Mapato ya Ndani.

Mradi mwingine upo Kijiji cha Bombo, ambapo ni Shule ya Msingi Kaghambe, na kumejengwa vyumba vya madarasa mawili na ofisi moja ambayo yamekamilika, na walipata sh. milioni 40 kupitia fedha za UVIKO 19.

Pia shule hiyo ina ujenzi wa vyumba viwili na ofisi moja, ujenzi upo kwenye madirisha. Mpaka sasa ujenzi huo ni nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo. Nguvu za wananchi ni sh. milioni 3.1, na Mfuko wa Jimbo ulitoa mifuko ya saruji na mabati vyenye thamani ya sh. milioni 2,080,000. Pia kuna mradi wa matundu 14 ya vyoo kwa walimu na wanafunzi na sh. milioni 2.9 zimetumika ikiwa ni nguvu za wananchi.

Shekilindi pia ameiomba Serikali kutoa sh. milioni 50 ili kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Bombo, ambapo hadi sasa wananchi wamejenga kwa nguvu zao na michango yao kwa sh. milioni 12,041,000, na zahanati hiyo ilianza kujengwa mwaka 2010 na mpaka sasa haijakamilika.

Naye Ofisa Elimu Kata ya Makanya Nelson Hizza alisema wananchi wa Kata ya Makanya pia hadi sasa wamejenga Kituo Shikizi kilichopo Kijiji cha Kweulasi ili kupunguza umbali kwa watoto waliokuwa wanasoma Shule ya Msingi Makanya, na kupunguza mrundikano kwa watoto waliokuwa wanasoma Shule ya Msingi Kwedau. Mfuko wa Jimbo umetoa sh. milioni 2.7 na wananchi sh. milioni 3.9.

Hizza alisema mradi mwingine uliopata fedha kutoka Serikali Kuu, ni ule uliopo Kijiji cha Kweulasi, ambapo Shule ya Sekondari Kweulasi ilipata sh. milioni 20 na kujenga chumba kimoja cha darasa, na kimekamilika.

Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu Bosnia (wa pili kushoto), akikagua ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi ya walimu Shule ya Msingi Mboghoi katika Kijiji cha Mdando, Kata ya Makanya, ambapo hadi kufikia usawa wa linta ni nguvu za wananchi. Kushoto ni Diwani wa Kata ya Makanya Zanuali Mohamed. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu Bosnia (kushoto), akisaidia kuchimba shimo la choo Shule ya Msingi Mboghoi katika Kijiji cha Mdando, Kata ya Makanya, (Picha na Yusuph Mussa).
Moja ya vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari Mdando, Kata ya Makanya, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ambavyo vilijengwa kwa fedha za Tozo, ambapo walipata sh. milioni 80 na kujenga madarasa manne na ofisi mbili za walimu. (Picha na Yusuph Mussa)
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu Bosnia (kushoto), akikagua ujenzi wa moja ya madaraja madogo yanayojengwa kwenye barabara kipande cha Kata ya Makanya. Barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha changarawe chini ya TARURA, ina urefu wa kilomita 72 kutoka Mlalo- Ngwelo- Mlola- Makanya- Milingano- Mashewa, na itagharimu sh. bilioni 3.5. Kulia ni Ofisa Mtendaji Kata ya Makanya Emiliana Kajula, na katikati ni Diwani wa Kata ya Makanya Zanuali Mohamed. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu Bosnia (kushoto), akizungumza na viongozi alioambatana nao mara baada ya kufika Shule ya Msingi Bosha iliyopo Kijiji cha Bwaya kujionea ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa vilivyokamilika. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu Bosnia (kulia), akimsikiliza Ofisa Mtendaji Kata ya Makanya, Emiliana Kajula (kushoto), akitoa maelezo juu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Kaghambe katika Kijiji cha Bombo. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu Bosnia (kushoto), akikagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Bombo, Kata ya Makanya. Shekilindi ameiomba Serikali kutoa sh. milioni 50 ili kukamilisha zahanati hiyo ambayo ujenzi wake umeanza 2010, huku wananchi wakiwa wamejenga kuanzia chini hadi kupaua. (Picha na Yusuph Mussa).