November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania waibuka na ushindi wa kishindo katika Mbio za Kimataifa za Kilomita 21 maarufu kama Tigo Kili International Half Marathon 2023

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online


WANARIADHA wa Tanzania wameng’ara kwa kwa kuibuka na ushindi wa kishindo katika Mbio za Kimataifa za Kilomita 21 maarufu kama Tigo Kili Half Marathon 2023 zilizofanyika Februari 26, mwaka huu katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika (MoCU) mjini Moshi.
Katika hizo, mshindi kwa upande wa wanaume Watanzania wakiongozwa na Emmanuel Giniki walishika nafasi nne za kwanza ambapo Giniki alitumia muda wa saa 1:00:36.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Josephat Gisemo aliekimbia kwa muda wa 1:05:12 akifuatiwa kwa Karibu na Decta Teziforce aliekimbia kwa muda wa saa 1:05:43 na kushika nafasi ya tatu.

Katika hotuba yake baada ya mashindano hayo Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa aliwapongeza washindi wa mbio hizo ambapo alisema mafanikio yao ymaeakisi matayarisho mazuri waliyoyafanya kabla ya kushiriki kwao.

“Ushindi wenu ni chachu kwa wengine kujiandaa vyema mwakani ili wafanye vizuri na kwenu itakuwa unawapa moyo wa kujituma Zaidi ili kulinda mafanikio mliyoapata”, alisema.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mary Masanja, Mchengerwa alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na waratibu na wadau wengine wa mbio hizo kutokana na umuhimu wake kwa Taifa.

“Mashindano haya ni muhimu kwa nchi yetu kutokana na ukweli ya kuwa mbali na kukuza kiwango cha michezo nchini pia yanachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya utalii hapa nchini”, alisema.

“Kutokana na mashindano haya kushirikisha na kuleta watu wengine kutoka mataifa zaidi ya 50 duniani kote, pia yanawezesha kutangazwa kwa vivutio vya utalii ukiwemo Mlima Kilimanjaro pamoja na kukuza utalii wa Zanzibar kwa kutangaza vivutio vilivyoko kisiwani humo”, alisema.

“Naomba kutumia nafasi hii pia kuwashukuru waandaaji na wadhamini wa mbio hizi kwa namna tulivyoshirikiana wakati nikiwa Waziri wa Utamaduni na Michezo na sasa kwa kweli naendelea kuona umuhimu wa tukio hili la kipekee katika sekta yetu ya utalii.”

“Hongereni sana kwani nimefahamishwa kuwa hii ni mbio ya 21 tangu kuanzishwa kwa mbio hizi maarufu; sisi kama serikali tunajivunia tukio hili ambalo linapeperusha bendera ya Taifa letu sio kimichezo tu, bali hata katika sekta ya utalii, kwani sasa hivi kila mtu duniani anazungumzia sports tourism na Kilimanjaro International Marathon kama mfano bora tukio la kimataifa linalotambulika kila mwaka”.

Aidha Waziri Mchengerwa aliwapongeza washindi wote katika mbio zote za Kilimanjaro Premium Lager km 42, Tigo Km21 na Grand Malt Km 5.
Aidha aliwapongeza wandaaji wa mashindano hayo kwa kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa ya kuyapandisha hadhi mashindano hayo ambayo kwa sasa yanajulikana kama Kilimanjaro Premium Lager International Marathon na hivyo kuzifanya mbio hizo kongwe kuliko zote hapa nchini ziendelee kuwa maarufu duniani kote na kuhusisha zaidi ya washiriki 12,000 kutoka mataifa zaidi ya 50.

Pia aliwapongeza wandaaji wa mbio hizo kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na chama cha riadha duniani (World Athletics) na kila cha hapa nchini (RT) kwa michango yao iliyochangia Kilimanjaro Marathon iendelee kuwa maarufu.

Waziri Mchengerwa pia aliwpaongeza wadhamini wote wa mio hizo wakongozwa na wadhamini wakuu Kilimanjaro Premium Lager kwa udhamini uliotukuka wa miaka 21.

Aidha aliapongeza wadhamini wengine ambao alisema ni pamoja na kampuni ya Tigo inayodhamini mbio za Km 21 na Grand Malt mbio za Km 5 maarufu kama Fun Run pamoja na wadhamini wengine ambao ni TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies na watoa huduma rasmi wakimemo Surveyed Plots Company Limited (SPC), GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel na CMC Automobiles na Salsalinero.

Aidha aliwaponheza wadau wengine ambao alisema ni pamoja na Chama Cha Riadha Tanzania, Baraza la Michezo Tanzania, Kamati ya Olympiki, Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MoCU), jogging clubs mbalimbali, Jeshi la Polisi, waratibu wa ndani waandaji Kilimanjaro Marathon Company Ltd, waratibu Executive Solutions na waadishi wa habari.

Afisa Mkuu wa Fedha kutoka Tigo,CPA. Innocent Rwetabura akimkabidhi mfano wa hundi,mshindi wa kwanza Tigo Kili International Half marathon(km 21) upande wa wanaume, Emmanuel Giniki