October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zoezi la kushushwa majini MV.Mwanza Hapa Kazi Tu limefanyika kwa asilimia 100

Na Judith Ferdinand, Timesmajira online, Mwanza

Meli mpya ya MV.Mwanza Hapa Kazi Tu, ambayo imefikia asilimia 82, imeshushwa ndani ya maji ambapo zoezi hilo limefanyika vyema kwa asilimia 100.

Huku Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL),imetakiwa kuendelea kusimamia mradi wa ujenzi wa meli hiyo ili ukamilike ndani ya muda uliopangwa na kuanza kuhudumia wananchi. Pamoja na kuhakikisha inasimamia miradi yote inayotekelezwa na serikali kama ilivyopangwa na kuleta thamani ya fedha iliowekezwa.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-Uchukuzi Atupele Mwakibete kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Profesa Makame Mbarawa,wakati wa hafla ya ushushaji wa meli ya MV.Mwanza Hapa Kazi Tu,iliofanyika Bandari ya Mwanza Kusini,jijini Mwanza.

Pia ametoa rai kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania kuhakikisha inajipanga kuendelea kuboresha Bandari katika Ziwa Victoria ili.meli hiyo iweze kutoa nanga bila shida wakati itakapoanza safari zake pamoja na gati lililopo mkoani Mara.

Mwakibete ameeleza kuwa, serikali imekuwa ikiwekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na MSCL kwa lengo la kuboresha huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya meli.

“Leo hii tunashuhudia ikishushwa kwenye maji,kazi nyingi za ujenzi wa meli tayari zimekamilika na ikiwa kwenye maji Mkandarasi anatarajiwa kukamilisha kazi chache zilizobaki na hatimaye meli iweze kukaguliwa na TASAC kabla ya kupewa cheti cha ubora ili kuruhusu iweze kuanza kutoa huduma ya usafiri,”ameeleza Mwakibete.

Ambapo kujengewa kwa meli hiyo kutasaidia kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha safari mpya zitakazosaidia kurahisisha shughuli za kibiashara,kikazi,utalii na safari binafsi kwenye maeneo mengi zaidi ya ilivyo sasa.

“Meli hii itakapo kamilika ndani ya mwaka huu siyo tu kutakuwa na ongezeko la meli bali pia usafiri huu,utakuwa umeboreshwa sana kwa vile meli itakuwa ya kisasa na yenye mwendo kasi mkubwa zaidi ya meli zilizopo,”ameeleza Mwakibete.

Sanjari na hayo Mwakibete ameielekeza Menejimenti ya MSCL kubainisha vijana waliopata utaalamu kupitia mradi huo waweze kutumika kadri ya mahitaji ya kampuni yatakavyojitokeza ili nguvu kazi yenye uzoefu isipotee.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL Erick Hamissi,ameeleza kuwa meli hiyo ikikamilika itahudumia bandari zote Kuu za Ziwa Victoria ikiwemo ya bandari ya Kemondo, Bukoba,Mwanza,Musoma na Portbell na Jinja za nchini Uganda pamoja na Kisumu nchini Kenya.

Hamissi ameeleza kuwa,meli hiyo ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu,ina uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo na magari madogo 20 hadi kukamilika kwake itagharimu kiasi cha bilioni 109.

“Wakati serikali ya awamu ya sita inapokea mradi huo ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 45 laki mpaka leo inavyoshushwa ndani ya maji imefikia asilimia 82, huku Mkandarasi ameishalipwa asilimia 88 sawa na bilioni 93.8,”ameeleza Hamissi.

Ameeleza kuwa meli hiyo itakuwa na madaraja sita ambayo ni VVIP itakayokuwa maalum kwa viongozo wa kitaifa ambapo watakuwa wanakaa watu wawili tu pamoja na viongozi wa kitaifa wa nchi jirani kama watapata kibali cha kusafiri na meli hiyo.

Huku ameeleza kuwa daraja la VIP ambalo litabeba watu mashuhuri sehemu hii itakuwa na watu wanne yaani vyumba vinne, daraja la kwanza litakalokuwa na watu 60, daraja la biashara litakalokuwa na watu 100 daraja la pili litakalokuwa na watu 200.

“Daraja la mwisho kwenye meli hii litakuwa ni la uchumi ambalo litakuwa linabeba abiria 834 na katika daraja hili kutakuwa na hadhi ya kisasa na wananchi watakaa kwa starehe na wataweza kufanya utali,”ameeleza Hamissi.

Ndani ya meli hii pia kutakuwa na buradani, kutakuwa na sehemu ya lift hasa kwa watu wenye changamoto ya kupanda ngazi na wagonjwa, na sehemu ya hospotali (dispensary) na sehemu ya wamama wajawazito.

” Tunatarajia meli hii itakuwa inatumia masaa 10 pekee kwenda bandari ya portbell nchi Uganda lakini pia itaenda Musoma mkoani Mara,” ameeleza Hamissi.

Muonekano wa Meli ya MV.Mwanza Hapa Kazi Tu,ikiwa inaelea ndani ya Ziwa Victoria, baada ya kushushwa majini,Bandari ya Mwanza Kusini.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kushuhudia ushushwaji wa meli ya MV.Mwanza Hapa Kazi Tu,zoezi lililofanywa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-Uchukuzi Atupele Mwakibete,Bandari ya Mwanza Kusini.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-Uchukuzi Atupele Mwakibete(katikati),akibonyeza kitufe kwa ajili ya kuanza kwa zoezi la ushushwaji wa meli ya MV.Mwanza Hapa Kazi Tu,lililofanyika Bandari ya Mwanza Kusini.