Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online Mwanza
Meli ya MV.Mwanza Hapa Kazi Tu, Februari 2023, inatarajiwa kushushwa ndani ya maji huku ikisubili kumalizika kwa kazi nyingine ambazo zinafanyika meli ikiwa kwenye maji.
Mpaka sasa mradi huo wa ujenzi wa meli hiyo umefikia asilimia 80 ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha bilioni 108.5.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari mkoani Mwanza,Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL),Edmond Rutajama,kwa ajili ya kutoa taarifa ya miradi inayotekelezwa na kampuni hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa MV.Mwanza Hapa Kazi Tu,ni mradi ambao Serikali ya awamu ya sita umeupokea kutoka katika serikali ya awamu ya tano.
Ambapo Serikali awamu ya sita ilipo pokea kijiti hicho mradi huo ulikuwa na asilimia 50 lakini sasa mradi huu umefikia asilimia 80.
“Katika moja ya hatua kubwa katika ujenzi wa meli kuna hatua ya pili ambayo itafikiwa mwanzoni mwa mwezi Februari ya kushushwa majini huku ikisubili hatua ya tatu ambayo ni kubwa la jaribio la mitambo ya kujaaribisha meli kama inaweza kutoka sehemu moja kwenda nyingine na namna mitambo ilivyofungwa na kila kitu,”ameeleza Rutajama.
Aidha ameeleza kuwa sababu ya kuchelewa kushusha ziwani tofauti na matarajio ya wengi ni masuala ya kiufundi ikiwemo muda wa zege kukauka ambao ni siku 45 hadi 60.Mv.Mwanza hapa kazi tu ni meli kubwa kuliko yoyote katika ukanda huu ambayo inatuheshimisha serikali na wananchi.
Inagharimu kiasi cha bilioni 108.5 hadi kukamilika kwa ujenzi wake Rutajama ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 serikali ilitenga fedha zaidi ya bilioni 113 kwa ajili ya MSCL kutekeleza miradi 12 ya meli ambapo kati yake miradi minne mipya, miradi miatano ya ukarabati na miradi mitatu ambayo inaendelea.
Katika miradi hiyo kiasi cha bilioni 53 zitakwenda katika miradi 7, iliopo Ziwa Tanganyika huku bilioni 57 zitakwenda katika miradi 5 iliopo Ziwa Victoria Mwanza na bilioni 2 zitatumika kuendeshwa meli ambazo wamepewa na Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) katika Ziwa Nyasa.
Ameeleza kuwa katika Ziwa Victoria watakuwa ujenzi wa meli mpya ya mizigo tani 3,000 na ukarabati wa meli ya MT.Nyangumi,meli ya msaada ya MT.Ukerewe pamoja na ujenzi unaendeleaje wa MV.Mwanza.
Ambapo mradi mwingine ni meli ya MV.Umoja ambayo ni ya mizigo ambayo kipindi inafanya kazi ilikuwa inafunguka milango ya biashara kati ya Tanzania na Uganda.
Meli ya MV.Umoja ukarabati wake umefikia asilimia 62 ambapo wanatarajia Machi 2023 itaanza kufanya kazi.Pia katika Ziwa Tanganyika watakamilisha ukarabati wa Mt.Sangara, ukarabati wa Mv.Liyemba ambayo ni meli kongwe kuliko meli zote pia wataikarabati na kurejesha meli ya MV.Muongozo.
“Meli ya mafuta ya MT.Sangara katika Ziwa Tanganyika ipo kwenye ukarabati ambapo Februari,mwaka huu tutakabidhiwa na kuanza kufanya kazi,”ameeleza Rutajama.
Pia watakuwa na ujenzi wa chelezo kubwa chenye uwezo wa kubeba tani 4,500, ujenzi wa meli ya mizigo ya tani 400 na itabeba abiria 600.
Aidha ameeleza kuwa vipaumbele vya kampuni hiyo ni kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na inaonesha matumizi halisi ya fedha zilizotolewa na serikali.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania