November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mpango akerwa na vitendo vya rushwa Mahakamani

Na Joyce Kasiki,Timesmajira Online,Dodoma

MAKAMU wa Rais Dkt.Philip Mpango amezindua maadhimisho ya wiki ya sheria nchini huku akionyeshwa kukerwa na vitendo vya rushwa kwa Mahakimu na Majaji na Mawakili.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimsho ya wiki ya sheria nchini Dkt.Mpango amesema  katika nyakati tofauti amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu muhimili wa Mahakama na vyombo vingine kama polisi na Magereza.

Dkt.Mpango amesema baadhi ya malalamiko hayo ni pamoja na  baadhi ya mahakimu,mawakili na majaji kutokuwa waaminifu kwa kudai rushwa kinyume cha viapo vyao .

“Mfano,kuna minada ya mifugo ambayo inakamatwa kwenye maeneo ya hifadhi  mara kadhaa,mfano Mbeya kule tumeletewa malalamiko, minada hiyo inazuiliwa kwa amri ya mahakama tena wakati mwingine unashituka kabisa hiyo mahakama imekaa jumapili ,au faini zinazoamriwa ni ndogo mno kwa hiyo mwenye mifugo yake analipa faini baada ya nusu saa anarudisha mifugo kwenye hifadhi ,

“Lakini pia nimepokea malalamiko ya fedha za kigeni ambazo zinakamatwa mipakani zinapotea mikononi mwa mahakama lakini pia wananchi wanalalamikia kwamba hukumu zinapindishwa ili kumpa ushindi mwenye fedha pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa kesi na kulipa gharama za mawakili .”amesema Dkt.Mpango

Vile vile amesema,wananchi wanalalamikia hukumu kuandikwa kwa lugha ya kingereza lakini pia watuhumiwa wanakaa mahabusu muda mrefu wanasubiri uchunguzi kukamilika huku wananchi wengine hawana  elimu ya sheria.

Pia Dkt.Mpango amesema,malalamiko mengine anayoyapokea kutoka kwa wananchi ni baadhi ya maeneo kutokuwa na mahakama hivyo hutembea umbali mrefu kutoka walipo wananchi mpaka mahakamani .

“Aidha wananchi wanalalamikia mila na desturi potofu zinazokinzana na sheria na hasa kuhusu mirathi na umiliki wa ardhi kwa wanawake na haki za watoto,mimi naamini changamoto hizi zinaepukika na kumalizwa kabisa.”

Ameutaka Muhimili huo wa Mahakama kuzikabili changamoto zote ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa lakini pia waendelee  kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha elimu mbadala ya usuluhishi inapatikana na kuendeleza utaratibu  wa maadhimisho ya kisheria ambayo yamekuwa yakitanguliwa na wiki ya sheria .

Maadhimisho hayo yalitanguliwa na maandamano kuanzia kituo Jumuishi cha Utoaji haki hadi uwanja wa Nyerere Square jijini Dodoma.