Na Cresensia Kapinga, TimesMajiraOnline,Ruvuma
WAKURUGENZI wa Halmashauri za Wilaya ya Nyasa na Mbinga zilizopo mkoani Ruvuma wamekemea vikali baadhi ya wazazi wenye watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, lakini hawajaripoti shule kwa visingizio mbalimbali.
Wamesema visingizio hivyo sio vya msingi hivyo wawapeleke shule haraka iwezekanavyo kabla mkono wa sheria haujawapitia.
Walitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea halmashauri hizo kwa lengo la kujua idadi ya wanafunzi wa elimu msingi wa darasa la awali na sekondari walioandikishwa na kuripoti shuleni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Jimson Mhagama alisema kuna wazazi wanatabia ya kuwapeleka watoto mashambani kwa lengo la kwenda kusaidia kulima vibarua au mashamba ya wazazi wao.
Alisema amewaagiza viongozi kuanzia ngazi ya shina hadi kata pamoja na watendaji wa vitongoji na vijiji kuendesha msako ambao utapita kila nyumba na watakao bainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema Halmashauri yake ilipangiwa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 4,452 lakini hadi Januari 17, mwaka huu wamepokea wanafunzi 2,100 sawa na asilimia 27.
Kwa upande wa elimu msingi kwa darasa la awali walitarajaia kuandikisha wanafunzi 5,484 lakini hadi jana wameandikisha watoto 5,444 sawa na asilimia 96 ya lengo.
“Hakuna sababu ya wazazi kuwakataza watoto wao wasiende shule kwani kupitia Serikali yetu ya awamu ya Sita inayoongoza na mama Samia inatoa elimu bure.
Lakini pia hatuangalii kipengele cha mtoto hana sale ya shule ama kiatu sisi tunachotaka mwananfunzi aje kuripoti akiwa na daftari pamoja na kichwa basi na si vinginevyo” alisema Mkurugenzi Mhagama.
Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Mbinga, Lucy Luwungo alisema kuwa walipangiwa jumla ya wanafunzi 2,721 wa kidato cha kwanza walioripoti hadi kufika Januari 16 walikuwa 1,147 sawa na asilimia 42.2 na ambao bado hawajaripoti ni 1,574 sawa na asilimia 57.8.
Alifafanua zaidi kuwa tayari wamejiwekea mikakati kwa wakuu wa shule zote za sekondari kutangaza maendeleo mbalimbali kama makanisani na msikitini kwa lengo la kuwakumbusha wazazi wawapeleke watoto shule.
“Kuna shule watoto 13 ndiyo walioriporti Shule ya Sekondari ya Dkt. Shein ipo Kata ya Mpepai kati ya watoto 242, kwa hiyo wasioriporti wapo 219 changamoto kubwa watoto wapo mashambani na wazazi wao.
Lakini pia tumeandika barua kwa maofisa watendaji na waratibu elimu kata wafuatilie hao wazazi wa watoto ambao hawajawaleta watoto shuleni na kuwapeleka mahakamani.” Alisema Luwungo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi