November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LATRA yaonya wamiliki wa mabasi wanaotoza nauli kubwa

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Kanda ya Magharibi imewataka wamiliki wa mabasi ya abiria kuhakikisha nauli zinazotozwa katika vyombo hivyo ni zile zilizoelekezwa na Mamlaka hiyo, kinyume na hapo watachukuliwa hatua kali.Hayo yamebainishwa jana na Afisa Leseni Msaidizi wa Mamlaka hiyo Kanda ya Magharibi Geofrey Mlambia katika mahojiano maalumu na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake.

Alisema baadhi ya wamiliki wa mabasi wamekuwa wakipandisha nauli kiholela hasa katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu na pindi wanafunzi wanaporejea shuleni wakitoka likizo.

Mlambia aliwataka wamiliki wa mabasi kuhakikisha nauli zinazotozwa katika vyombo vyao ni zile zilizoelekezwa na Mamlaka hiyo na tiketi zinazotolewa pia ziwe za mtandao, alionya kuwa basi lolote litakalobainika kutoza nauli zaidi au kutotoa tiketi za mtandao mmiliki atapigwa faini ya sh 250,000 na kurudisha nauli zilizozidi.

Alitoa mfano wa nauli kutoka Tabora-Dar es salaam kuwa ni sh 46,000 kwa mabasi ya Semi Luxury na sh 40,000 kwa mabasi ya kawaida, na kubainisha kuwa nauli hizo zimebandikiwa katika mabasi yote, ili abiria wasiibiwe fedha zao.

‘LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani tutaendelea kufanya doria na ukaguzi wa kushutikiza mara kwa mara katika mabasi yote ili kubaini wanaokaidi maagizo hayo na kuchukua hatua mara moja’, alisema.

Akizungumzia maeneo ambayo hayana huduma za usafiri katika Manispaa ya Tabora na maeneo mengine aliwataka wamiliki wa daladala kuchangamkia fursa hiyo kwa kufika Ofisi za LATRA ili kuomba ruti za maeneo hayo.

Aidha aliwataka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji kwa kuacha kubeba mizigo kupita kiasi au kuchanganya mizigo na abiria kwani hilo ni kosa kisheria na hatua kali zitachukuliwa ikiwemo kupigwa faini ama kufungiwa chombo.

Baadhi ya mabasi ya abiria yakiwa stendi tayari kwa ajili ya kupakia abiria ili kuwasafirisha katika Mikoa mbalimbali hapa nchini.