Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MADIWANI wa halmashauri ya manispaa Tabora wamempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kasi kubwa ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Wakiongea kwa nyakati tofauti katika kikao cha bajeti cha baraza hilo kilichofanyika juzi katika ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo walisema serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia imewatendea haki wananchi.
Walibainisha kuwa miradi mingi katika manispaa hiyo ilikuwa inasuasua kutokana na ufinyu wa bajeti lakini baada ya kuingia madarakani Rais amemwaga fedha katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, barabara, maji na nyinginezo hivyo kuongeza kasi ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta hizo.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela ambaye ni diwani wa kata ya Isevya alisema Rais Samia kila siku anafanya jambo jipya linalogusa maisha ya wananchi hali inayopelekea kutatuliwa kero zao.
Aliongeza kuwa halmashauri hiyo haijawahi kupata asilimia 100 ya makadirio ya bajeti yake ya maendeleo lakini chini ya uongozi wa Rais Samia wameletewa fedha zote walizoomba na kufanikisha utekelezaji mipango yao ya maendeleo.
‘Tunamkushukuru sana Rais kwa kutuletea zaidi ya bil 1.5 za ujenzi wa hospitali ya wilaya huduma sasa zinatolewa, pia sh bil 1 kwa ajili ya jengo la utawala na kila mwezi anatuletea fedha za mfuko wa Jimbo na za matumizi mengineyo’, alisema.
Aidha alipongeza hatua ya Rais Samia kuanza kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima kwa kuwapunguzia gharama kutoka sh 140,000 hadi sh 70,000 tu kwa mfuko wa mbolea na kubainisha kuwa itawasaidia kuongeza uzalishaji mazao yao.
Mstahiki Meya pia alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo na Menejimenti yake katika kusimamia miradi ya maendeleo ila akasikitishwa na tabia ya baadhi ya watendaji kuwanyanyasa mamantilie.
Naye Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini Emanuel Adamson Mwakasaka alimshukuru Rais kwa kuwaongezea bajeti Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) hali iliyopelekea barabara na madaraja kutengenezwa katika kata zote.
Ili miundombinu hiyo idumu alishauri watendaji wa vijiji na kata kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha magari yenye uzito mkubwa hayapitishwi katika madaraja na barabara hizo na ikibidi ziwekwe alama za uzito wa magari.
Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo Seif Salumu alisema wataendelea kusimamia utekelezaji miradi yote kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha thamani ya fedha (value for money) inaonekana ili kuwanufaisha wananchi.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â