Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Salha Burian amewataka Viongozi wa Vyama Vikuu wa Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani hapa kukutana na Viongozi wa AMCOS na kushughulikia changamoto zao.
Ametoa ushauri huo juzi alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa 30 wa Mwaka wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU 2008 LTD) uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Mjini hapa.
Alisema kero nyingi zinazowakabili wakulima zinatokana na Viongozi wa Vyama Vikuu kutokuwa na utaratibu wa kutembelea wakulima ili kujua changamoto walizo nao na kuzitafutia ufumbuzi mapema ili kutokwamisha shughuli zao.
RC alisisitiza kuwa weledi na uadilifu wa Viongozi wa Ushirika ikiwemo ushirikiano mzuri na Viongozi wa vyama wa msingi (AMCOS) ndiyo msingi mkuu wa mafanikio ya wakulima.
‘Ni jukumu la Watendaji wa Vyama Vikuu vya Ushirika kutembelea wakulima ili kujua changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kabla ya msimu mpya wa kilimo kuanza, sio kusubiri wakikaribia kuvuna mazao ndiyo muwatembelee’, alisema.
Alitaja manufaa ya ushirika kuwa ni kuwaweka pamoja wakulima na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa weledi mkubwa ikiwemo kuwatafutia masoko ya uhakika.
Aidha Balozi Batilda aliwataka kuendelea kutoa elimu ya kilimo bora ili kuchochea uzalishaji mazao mengi ambayo yatawawezesha kujiongezea kipato huku akiwaonya kutotumikisha watoto wao katika kazi hiyo.
Ili kuhakikisha mazingira ya Mkoa huo yanaendelea kuwa bora alisema wameanzisha utaratibu ambapo kila mtoto anayezaliwa atapandiwa mti katika eneo lililoandaliwa na wazazi kutakiwa kuutunza hadi atakapokua.
Kwa upande wake mkulima mkazi wa Kijiji cha Isila ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani hapa Said Ntahondi alishauri serikali kuzibana kampuni zinazonunua tumbaku ya wakulima kutochelewesha malipo yao.
Alipongeza juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6 chini ya uongozi shupavu wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika ya mazao yao na kuuza kwa bei nzuri.
More Stories
RC Chalamila awataka ndugu,Jamaa na marafiki kuwa wavumilivu zoezi la uokoaji likiendelea
Baraza la Madiwani lafukuza watumishi wawili idara ya afya
Wanasheria waombwa kusaidia kusimamia sheria, sera ulinzi wa taarifa