November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkandarasi aliyepewa tenda kusambaza umeme wa Rea Mbeya aonywa

Na Esther Macha,Timesmajira, Online Mbeya

MKURUGENZI mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ,Mhandisi Hassan Saidy amemwonya mkandarasi wa Kampuni ya Derm limited ya Jijini Dar es Salaam, Peter Mbwambo kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huo ambao utanufaisha wakazi zaidi ya 3,000 katika Mkoa wa Mbeya ambao utahusisha vituo 59 mijini na vijijini kwa gharama ya Sh 10.5 bilioni fedha zilizotolewa na Serikali ya awamu ya sita.

Mkurugenzi huyo alitoa angalizo hilo jana Mbele ya Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini ,Dkt. Tulia Ackson mara baada ya kuzindua mradi wa usambazaji umeme wa Rea sambamba na kutoa mkataba wa kazi kwa mkandarasi.

“Mkandarasi tambua kuwa kuwa mradi huu umeelekezwa na Serikali na isitokee ukaunganishwa kwa watu ambao hawajaingizwa kwenye mpango kwani kumekuwepo na changamoto kubwa sana za uendeshaji wa miradi ya Rea kwa wakandarasi wanaopewa zabuni ”amesema.

Ameongeza kuwa “Tumekuja mkoani Mbeya kwa ajili ya jambo moja kubwa ikiwepo kutetekeza ombi la Spika wa Bunge la utekelezaji wa mradi wa umeme kwa wananchi wake ambalo aliliwasilisha kwenye vikao vya Bunge na Serikali kuridhia na kutoa Sh 10.5 bilioni ”,amesema.

Amesema kuwa mradi huu si kwa Vijijini pekee bali utagusa na wananchi wa kata za pembezoni kutokana na kusafirishwa umbali wa kilometa 150 jambo ambalo litaondoa changamoto kwa wananchi kulala giza.

Kwa upande wake Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini ,Dkt Tulia Ackson amesema kuwa uwepo wa mradi huo utachochea shughuli za kiuchumi ikiwepo ufugaji,vinywaji baridi na viwanda vidogo vidogo.

“Miradi yote ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2020/21 ambapo tuliwahaidi mambo kadhaa ikiwepo ,maji ,elimu,afya na miundombinu ya barabara ambapo sasa Serikali zinatarajia kuingia mkataba wa njia nne kutoka Uyole mpaka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA) yenye urefu wa kilometa 32.

“Ni lazima tuwaeleze wananchi utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020/21 na leo hii mnawaona wabunge wengine wameshiriki uzinduzi wa mradi wa REA na Majimbo yao inatekelezwa yote hii ni kupiga mwingi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ”amesema.

Kwa upande wake Mhandisi wa mradi huo Peter Mbwambo amesema anatarajia kukamilisha kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo Desemba mwaka huu utakuwa umekamilika.

“Gharama za mradi ni Bilioni 10.5 ni wa kipindi cha miezi 18 lakini sisi tunatarajia mwaka 2024 huku sehemu ya ajira za muda mfupi zitatolewa kwa vijana wazawa ”amesema.

Mhandisi, Mbwambo amesema baada ya kutekeleza mradi huo wanatarajia vijana wengi watakuwa na ujuzi ambao watatakiwa kujiendeleza kidogo VETA kwa lengo la kupata vyeti.