November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 96.1 waliofanya mtihani wa marudio wa kumaliza elimu ya msingi wafaulu

Na Mwandishi wetu ,Dar es Salaam

JUMLA ya wanafunzi 2,095 kati ya 2,180 waliofanya mtihani wa marudio wa kumaliza elimu ya msingi kati ya Desemba 21 na 22 mwaka 2022 wamefaulu daraja A hadi C sawa na asilimia 96.1.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Januari 4,2023 jijini Da es Salaam Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Athumani Amasi wakati akitoa taarifa ya matokeo ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne na kidato ca pili uliofanyika Oktoba na Novemba mwaka jana.

Amasi amesema wanafunzi hao kati ya 2,194  walifutiwa matokeo ya mtihani huo na Necta baada ya kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu katikati mtihani uliofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka jana.

Hata hivyo Amasi amesema kati ya wanafunzi hao 2,194 waliofutiwa matokeo waliofanya mtihani ni 2,180, wachache hawakushiriki mchakato huo kwa sababu mbalimbali, akisema huenda wengine walikwenda nje ya nchi.

“Watoto hawa walisababishiwa kufanya vitendo vya udanganyifu, siyo kwamba hawana uwezo. Uwezo wanao tena mzuri lakini kwa sababu wanazozijua wenyewe wanawapa majibu ya mtihani na kuwaharibu watoto hawa.

“Wanawaondolea hali ya kujiamini katika jamii kwamba bila kupewa majibu hawafaulu wakati wana uwezo na mtihani huu wa marudio walioufanya wamesimamiwa na Necta na wamefanya vizuri na ufaulu mzuri,” amesema Amasi.

Amasi amewataka watu wanaowapa majibu wanafunzi kuacha tabia hiyo, akisema wanaharibu Taifa na elimu kwa malengo binafsi sambamba na kuwaondolea hali ya kujiamini wanafunzi hao.

“Tuwaache watoto wafanye mtihani wenyewe na tuwafundishe vizuri ili waweze kufaulu, kama ambavyo umeona wamefanya vizuri bila usaidizi,” amesema Amasi.

Kwa mujibu wa Amasi, matokeo ya wanafunzi hao yatawasilishwa kwenye mamlaka husika ili ifanye uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na elimu ya sekondari kwa mwaka huu wa 2023.

Aidha amesema baraza hilo la mitihani linazipongeza kamati za uendeshaji mitihani za mikoa, halmashauri, manispaa pamoja na wakuu wa shule, wasimamizi na wasahihishaji wa upimaji huo kwa kazi kubwa waliofanya katika kutekeleza jukumu hilo.